Kampuni 11 za Tanzania zaanza kunufaika biashara AfCFTA

Dar es Salaam. Kampuni 11 za Tanzania zimeanza kunufaika na ufanyaji wa biashara katika Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

Kampuni hizo zimeanza kutumia fursa kwa kusafirisha bidhaa za kahawa, katani, viungo, karanga na tumbaku kwenda nchi mbalimbali Afrika ikiwemo Nigeria, Ghana, Algeria na Morocco.

Hayo, yamebainishwa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Julai 3, 2024 katika uzinduzi wa Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), huku akisisitiza kuendelea kuhamasisha wengine kutumia fursa huyo.

“Serikali itaendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara na kwa wizara milango iko wazi kusaidia wafanyabiashara,”amesema Samia.

Pia aliwataka washiriki wa maonyesho ya Sabasaba watumie fursa hiyo kujifunza na kujipanga kuhudumia masoko makubwa ya ndani, kikanda na kimataifa.

Aliwataka wafanyabiashara hao kufika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kujisajili ili kutumia fursa ya kuuza bidhaa zao katika soko la AfCFTA.

Mbali na hilo, Rais Samia amesema uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Msumbiji ulianza miaka mingi kupitia mitandao ya kibiashara katika pwani za nchi hizo na kuibuka kwa miji mikubwa ya kibiashara kuanzia Mogadishu kupitia Kilwa hadi Sopala Msumbiji.

Amesema mbaki na waasisi ambao ni Marais wa nchi hizo, viongozi waliofuata waliendeleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo na ujio wa nyusi umeimarisha dhamira hiyo.

“Waandaaji wa maonyesho, Dk Ashantu Kijaji ambaye nimembadilisha kazi jana kabla ya leo ila natambua kazi kubwa aliyoifanya katika kutayarisha maonyesho haya katika kujenga wizara ya viwanda na bishara,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo amesema wataendelea kuboresha maonyesho hayo mwaka hadi mwaka ili washiriki wanaokuja wavutiwe kurudi tena.

Rais Samia ameshukuru kuliona Banda la Mama Mkapa likiwa bado imara kwani alionana naye akiwa ofisa mdogo wa banda hilo.

Amesema maonyesho haya ni nyenzo katika kuchochea maonyesho mbalimbali ya sekta za kiuchumi tangu 1963 ambayo yamejizolea sifa nyingi barani Afrika na duniani kwa ujumla na kauli mbiu yake ikiwa, ‘Tanzania ni mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji.’

Katika Kampuni zilizoshiriki amesema inaonyesha ukuaji mkubwa ndani ya kanda na kwingineko kimataifa na Dar es Salaam na  hilo limechochewa na juhudi za kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani kwenye nyanja za biashara viwanda na uwekezaji.

Kwa hiyo njia ya kufikia azma hiyo ni uendelezaji na uimarishaji wa ushirikiano wa kitaifa kikanda na kimataifa ili kufungua fursa za biashara na uwekezaji.

Related Posts