Kigoma. Mwenyekiti wa Kijiji cha Pamila, Wilaya ya Kigoma, Obedi Tuwazaniwe ameeleza namna tope linalozaniwa kuwa volcano lilivyozua taharuki kwa wakazi wa kijiji hicho, huku mtaalamu wa jiolojia mkoa akiwatoa hofu wananchi.
Tuwazaniwe amezungumza jana Julai 2, 2024 mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ilikwenda kujionea hali halisi kwenye eneo hilo.
Alisema tope hilo lilianza polepole lakini ilipofika mwishoni mwa wiki iliyopita liliongezeka na kufunika eneo kubwa la bonde la Nyankara na kuibuka uji mzito unaodhaniwa ni volcano.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Pamila, Peter Edward amesema taarifa zinaonesha hali hiyo ilianza baada ya mtu mmoja aliyeanzisha bwawa la kufuga samaki katika eneo hilo.
Inaelezwa kuwa samaki wote walikufa na katikati ya bwawa alilokuwa akilitumia kufugia samaki kisha kukaibuka kichuguu kikubwa.
Amesema baada ya muda, kichuguu hicho kiliongezeka na kuwa na mchanga wenye maji maji sawa na tope zito, hivyo watu wengi kuanza kupata hofu kwamba huenda eneo hilo likalipuka volcano kama inavyotokea maeneo mengine hivyo kulazimika kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali.
Akizungumzia hali hiyo, Mtaalam wa Miamba na Jiolojia kutoka Ofisi ya Madini Mkoani Kigoma, David Ndosi alikiri kuwa hiyo ni volcano ya mchanga na maji, ambayo kitaalamu inaitwa ‘Sand Eruption Volcano’.
Amesema huo ni mchanganyiko wa tope na maji huku akisema huwa haina moto kama zilivyo volcano nyingine zinazojulikana kwa watu wengi.
Ndosi amesema mara nyingi volkeno kama hiyo hutokea maeneo yenye bonde la ufa na matetemeko ya ardhi kutokana na miamba kutikiswa.
Kutikiswa huko huwa kunasababisha mchanga na chembe chembe za maji zinazotengeneza tope kupanda juu, kama ilivyotokea katika eneo hilo.
Amesema tope hilo halina madhara lakini wananchi wanapaswa kukaa mbali nalo kwa sababu wanaweza kuzama na kupoteza maisha huku akieleza kuwa uchunguzi zaidi wa kimaabara utafanywa kujua sababu hasa ya kilichotokea.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Utunzaji Mazingira (NEMC), Edith Makungu amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kali, wamefika eneo la tukio na kuchukua sampuli za maji na udongo kwa ajili ya uchunguzi ili kujua kama yana madhara au hayana.
“Lakini tutachukua sampuli ya maji ili tujue haya maji yana kemikali za aina gani ambazo zinaweza kuleta madhara kwenye mashamba au kwa binadamu sababu eneo hili ni eneo la kilimo lakini pia kuna vyanzo vya maji mbalimbali ambavyo vinaenda kwa wananchi,” amesema Makungu.
Huku akiwatoa hofu kuwa tope hilo halina madhara, Kali amewatahadharisha wananchi wanaoishi kuzunguka Bonde la Nyankara kukaa mbali na eneo hilo linalodaiwa kuwa tope hilo linatembea wakati huu ambao wataalamu wanaendelea kufanya uchunguzi.