Huyu hapa mrithi wa Chama Msimbazi

KLABU ya Simba imefikia makubaliano ya kumsajili aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Stella Adjame ya Ivory Coast, Jean Charles Ohoua kwa kandarasi ya miaka miwili.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast ametambulishwa ndani ya kikosi hicho ukiwa ni muda mfupi tu tangu aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, Mzambia Clatous Chama kujiunga na Yanga baada ya mkataba wake kuisha huku kukiwa hakuna mazungumzo mapya.

Ohoua ndiye anayetazamwa kama mrithi wa Chama baada ya msimu uliopita kuibuka mchezaji bora (MVP), wa Ligi Kuu ya Ivory Coast alikofunga mabao 12 na asisti tisa  na kuwavutia mabosi wa Msimbazi walioinasa saini yake.

Usajili huo unakuwa wa nne katika timu hiyo baada ya kuwatambulisha beki wa kati, Lameck Lawi aliyetokea Coastal Union, winga Mzambia Joshua Mutale (Power Dynamos) na mshambuliaji Mganda Steven Dese Mukwala aliyetoka Asante Kotoko ya Ghana.

Upande wa mastaa waliotemwa hadi sasa ni aliyekuwa nahodha wa timu hiyo John Bocco, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, Shaaban Idd Chilunda, Luis Miquissone, Kennedy Juma na Henock Inonga aliyetua FAR Rabat ya Morocco huku Chama akijiunga na Yanga.

Related Posts