Makambako. Uzalishaji wa mipira ya mikononi (glovu) katika Kiwanda cha Idofi cha Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kilichopo Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe, umeiwezesha Serikali kutoa ajira kwa vijana 150, huku ikiokoa Sh20 bilioni kwa mwaka zilizokuwa zikinunua kifaa tiba hicho nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano Julai 3, 2024 na Kaimu Meneja wa kiwanda hicho, Shiwa Mushi baada ya wahariri wa vyombo vya habari kutembelea kiwandani hapo kuona namna kinavyofanya kazi.
Mushi amesema hadi sasa wamewapa ajira za kudumu na zisizo za kudumu wafanyakazi takribani 150, huku lengo likiwa ni kutoa ajira 200 kwa vijana.
Hata hivyo, amesema awali Serikali ilikuwa inaagiza glovu nje ya nchi kwa asilimia 100, lakini uzalishaji huo ulioanza takribani miezi sita sasa utaokoa fedha za Serikali Sh20 bilioni kwa mwaka.
Mushi amesema mahitaji ya mipira ya mikono nchini ni jozi milioni 104 kwa mwaka, lakini kiwanda hicho kinazalisha milioni 86 ya mahitaji hayo, hivyo uagizaji kupungua.
“Tunasambaza mipira ya mikononi katika vituo vya afya vya Serikali na vile vya binafsi ambavyo vimesajiliwa,” amesema Mushi.
Amesema kiwanda hicho kilichoanza uzalishaji Februari 12, 2024 baada ya kuzinduliwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango Oktoba mwaka jana, kinazalisha jozi 10, 000 kwa siku na malengo kuzalisha jozi 20,000.
Mbali na kiwanda hicho kilichoanza ujenzi wake kipindi cha mlipuko wa ugonjwa Uviko-19 ambacho glovu na barakoa zilitumika zaidi, ili kujikinga na virusi vya ugonjwa huo, MSD inamiliki viwanda viwili vya vifaa tiba vilivyopo mikoa ya Simiyu na Pwani.
Mfanyakazi wa kiwanda hicho katika kitengo cha ufuaji na ukaushaji glovu, Plackseda David amesema tangu kiwanda hicho kimeanza uzalishaji, kazi zinafanyika vizuri.
“Changamoto katika kitengo hiki hakuna labda kama mtambo utazimika ghafla, lakini ni nadra sana,” amesema Plackseda.
Mfanyakazi mwingine, Elijusi Msovela katika kitengo cha ufuaji, amesema uwepo wa kiwanda hicho umewasaidia kupata ajira na kuboresha maisha yao.
“Huu mwezi wa nne tangu nianze kazi kiwandani hapa, kuna manufaa makubwa katika majukumu yangu ya kila siku kwa kuwa naweza kujihudumia,”amesema Msovela.
Hata hivyo, ameishauri Serikali kuogeza uwekezaji wa viwanda, ili kuendelea kutoa ajira kwa vijana.
Meneja wa MSD Kanda ya Iringa Robert Lugembe amesema kanda hiyo inahudumia mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa na Njombe.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano MSD, Etty Kusiluka amesema kabla ya kuanza uzalishaji MSD ilikuwa mdau mkubwa wa kununua vifaatiba hivyo.
Akizungumza katika ofisi za kanda za MSD Iringa jana, Lugembe amesema kwa kawaida wanapokea oda za vifaatiba na dawa kwa wateja kuanzia tarehe moja hadi kumi kila mwezi.
“Mfano mteja ukikamilisha oda yako ndani ya tarehe hizo, tarehe 11 tunaanza kupeleka dawa na vifaatiba na dawa,” amesema Lugembe.
Amesema katika halmashauri 17 za kanda hiyo wanazohudumia wanakwenda kuzitembelea mara sita kwa mwaka.