Morogoro. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro, Joanfaith Kataraia amethibitisha kukamatwa kwa watumishi wawili wanaodaiwa kuhujumu miradi ya maendeleo wilayani hapo huku akisema hatua inayofuata ni kufikishwa mahakamani.
Juni 30, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, akiwa kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kujadili na kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliagiza kukamatwa kwa watumishi hao wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa madai ya kuhujumu miradi hiyo ya maendeleo na kusababisha upotevu wa fedha za umma.
Malima aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watumishi hao ili wajibu tuhuma zinazowakabili.
Alisema hayuko tayari kuona fedha za Serikali zinazotumika kutekeleza miradi hiyo zikiangamia kisa tu kuna watumishi wabadhilifu.
Hata hivyo, Mwananchi Digital imemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro, Alex Mkama kuhusiana na hilo na amesema bado hajapata taarifa kama watendaji hao wameshakamatwa.
“Wakati Mkuu wa Mkoa (Malima) anatoa maagizo ya kukamatwa kwa watendaji hao mimi sikuwepo, lakini hata hivyo sijapata taarifa kutoka kwa maofisa wangu kama wamekamatwa, ngoja nifuatilie nitakujulisha,” amesema Mkama.
Akizungumza na Mwananchi leo, Julai 2, ofisini kwake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro, Joanfaith Kataraiya amesema watumishi hao wameshakamatwa na utaratibu wa kuwafikisha mahakamani unaendelea.
“Tumepokea agizo la Mkuu wa Mkoa kuwakamata watumishi ambao wanadaiwa kuhusika na upotevu wa fedha za miradi ya maendeleo. Maelekezo hayo yameshafanyiwa kazi kwa kukamatwa kwa watumishi hao,” amesema Kataraiya.
Amesema Mkuu wa Mkoa alisisitiza watumishi hao wakishakamatwa tukubaliane nao namna ya kuzilipa fedha hizo aidha mbele ya Jeshi la Polisi au mahakamani.
Amesema lengo ni kurejesha fedha hizo ambazo ni stahiki ya serikali.
“Tulikuwa na watumishi wengi ambao tuliagizwa washikiliwe na tuweze kupata muafaka wa namna watakavyorejesha hizo fedha. Kwa kiasi kikubwa tumeshawakamata na kuna ambao tumefanya nao mazungumzo na kupata suluhu ya namna watakavyorejesha fedha za Serikali,” amesema Kataraiya.
Amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kuweka mbele uadilifu na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuwasababishia kujihusisha na upotevu wa fedha wanaposimamia miradi huku akisema maadili yanaanzia kwao.
Awali, Mkuu wa Mkoa alitaja watumishi waliotakiwa kukamatwa kuwa ni pamoja na Mtendaji Kata ya Mkulazi, Yasin Mohamed anayedaiwa pia kutelekeza pikipiki ya Serikali na mwingine ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kasanga, John Msami anayedaiwa kufanya ubadhilifu wa Sh18 milioni fedha ambazo ni mapato ya halmashauri hiyo.
Joseph Josephat, mkazi wa Halmashauri ya Morogoro, amepongeza hatua ya Mkuu wa Mkoa kudhibiti upotevu wa fedha za umma. “Watumishi wengi hawana maadili kwenye kazi wanazofanya, hivyo kitendo cha Mkuu wa Mkoa kutangaza wakamatwe kinaashiria kuwa anao uchungu na fedha za Serikali. Wabadhilifu wote wachukuliwe sheria bila kujali vyeo vyao,” amesema Josephat.