Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amewakubali na kuwapokea mawakili wapya 555 na kuwasajili katika daftari la mawakili nchini, huku akiwaonya mawakili wenye utovu nidhamu.
Pia, amekitaka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuwasimamia wanachama wake ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na uaminifu katika utoaji haki nchini.
Profesa Juma ametoa agizo hilo, leo Jumatano, Julai 3, 2024 jiji Dar es Salaam, baada ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wa kujitegemea 555 kwenye sherehe za 70 tangu kuanzishwa kwake.
Mawakili hao wamefikia hatua hiyo, baada ya kuhitimu mafunzo ya uwakili katika Shule ya Sheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania) na kuthibitishwa na Jaji Mkuu.
Profesa Juma ametoa kauli hiyo, baada ya ofisi yake, ofisi ya Jaji Kiongozi na Majaji Wafawidhi kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya vitendo vya utovu wa maadili vinavyofanywa na mawakili huku akitoa mifano kadhaa ya malalamiko wanayopokea.
“Ni aibu kubwa kwa wakili kupanga na kufungua ofisi, halafu anakataa kulipa kodi ya pango kwa sababu yeye ni wakili,” amesema Profesa Juma.
“Hivyo, nawaomba majaji tuanze kutumia mamlaka yetu kwa niaba ya wananchi, chini ya Sheria ya Mawakili, kama Kamati na Chapter hizi hazitafanya kazi zake. Tusipofanya hivyo siyo tu heshima ya TLS itashuka, bali pia heshima ya Mahakama nayo itashuka,” amesema.
Alifafanua kuwa Mahakama ya Tanzania haitakuwa tayari kufumbia macho vitendo vya utovu wa nidhamu vya mawakili, huku akiziagiza Kanda (Chapter) za TLS na Kamati ya Kitaifa ya Maadili ya chama hicho kufanya kazi yake kikamilifu.
“Maadili ndiyo yatadumisha taaluma ya uwakili, uanasheria. Mkiweza kusimamia maadili nyinyi wenyewe hakuna mtu yoyote ambaye atawaingilia. Utadumu kwenye taaluma ya uwakili kama utakuwa mwadilifu,” amesema.
“Nataka mkasimamie maadili kwelikweli, kamati ya taifa ya TLS ifanye kazi na isipofanya kazi, majaji tutatumia mamlaka yetu chini ya sheria za mawakili,” amesema.
Amesema kila taaluma au chama, mfano Chama cha Mawakili Tanganyika wana kanuni zinazosimamia maadili, hivyo aliwataka kanuni hizo ziwaongoze katika shughuli zao za kila siku.
“Kama taratibu za taaluma yenu zilivyo, kila wakili anatakiwa kujiunga katika Chapter, ambazo ndiyo husimamia maadili yenu na kuwasilisha taarifa kwenye Kamati ya Kitaifa ya Maadili kama kuna Wakili anaenda kinyume na maadili ya kazi yake,” amesema na kuongeza
“Mahakama kama mwakilishi wa wananchi itahakikisha maadili yanasimamiwa ipasavyo kama jukumu hilo halitatekelezwa kikamilifu na Chapters na Kamati ya Kitaifa ya TLS” amesema.
Profesa Juma ametoa mifano michache ya utovu wa maadili kwa mawakili ni pamoja na wakili kukataa kurudisha kwa mteja wake nyaraka halisi za shauri.
“Nyaraka zote za shauri ni mali ya mteja, hivyo anapobadilisha wakili au mkataba unapoisha zile nyaraka lazima zirudi kwa mteja husika na siyo mali yako,” ameonya.
“Wananchi wamekuja kulalamika kwetu, wakisema kwamba hawana kumbukumbu ya mashauri yao kwa sababu wakili amekataa kuwarudishia majalada na wangependa kupata wakili mwingine. Huo ni utovu wa nidhamu na itakuwa vizuri utovu wa aina hii ushughulikiwe na Chama cha Mawakili wenyewe,” amesema.
Mfano mwingine ni wakili kusimamia mkataba wa mauziano ya shamba na kupokea sehemu ya malipo na baadaye kupotea: “Hizi siyo hadithi za kutungwa, tunapokea hayo malalamiko. Mteja anakuja kuuliza unakuwa mkali.”
Amendelea kutoa mifano ya malalamiko wanayokutana nayo ni wakili kushindwa kulipa kodi ya pango kwa mwenye nyumba.
“Kuna lalamiko kwamba wakili aliwasilisha hati ya maridhiano mahakamani akisema wadaawa wamekubaliana kulipana nje ya Mahakama, lakini wahusika hawajui. Wakili kutohudhuria mahakamani licha ya kulipwa, unachukua fedha huonekani, wakati mwingine kesi inafutwa. Hilo ni kosa la kimaadili,” aliongeza.
Hafidh Suleiman Kusoya ni mmoja wa mawakili wapya waliopokewa na kukubalika, ambapo amesema haki bila maadili haiwezi kutendeka.
“Taaluma ya sheria msingi wake mkubwa ni maadili, hivyo bila kuwa na maadili hatuwezi kufanya kazi yetu kwa uadilifu na kuweza kutenda haki,” amesema.
Kwa upande wake, wakili mpya, Benita Mpento amesema suala la maadili ni jambo wamefundishwa kuanza walipoanza kusoma hadi wanamaliza, hivyo walishaandaliwa kufanya kazi kwa uadilifu na maadili.