Malinyi. Mwanafunzi Hamisi Haji, mkazi wa Mtimbila Wilaya ya Malinyi mwenye ulemavu wa viungo, ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kumsaidia aweze kuendelea na masomo ya kidato cha tano.
Mtoto huyo anatumia vidole vya miguu kuandika na kufanya shughuli nyingine na amefaulu kidato cha nne na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano, lakini amekosa matumaini ya kuendelea na masomo yake kutokana na ukosefu wa fedha na mahitaji muhimu kutoka na hali duni ya familia yake.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Juni 3, 2024, Haji amesema alizaliwa na ulemavu wa mikono na miguu na kiungo pekee kinachomsaidia kufanya kazi ndogo ndogo kama kula na kuandika ni miguu yake.
Kwa sasa anaishi na bibi yake baada ya mama yake mzazi kufariki dunia akiwa darasa la tatu.
“Mimi nilizaliwa na hali ya ulemavu wa mikono na miguu, mikono haifanyi kazi kabisa lakini miguu inanisaidia kufanya kazi ndogo ndogo ikiwemo kula, kuandika na kazi zingine lakini mikono yangu haiwezi kufanya chochote. Kazi zingine kama kuoga na kufua nimekuwa nikisaidiwa hapa nyumbani na mdogo wangu pamoja na bibi,” amesema Haji.
Amesema alipokuwa anasoma alikuwa anapata shida kwa sababu shule aliyokuwa anasoma ilikuwa mbali na nyumbani, lakini baadaye alipofika kidato cha nne alipata msaada wa kuhamishiwa shule na ofisa elimu wilaya na kupelekwa shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu Kilosa alikohitimu kidato cha nne na kupata ufaulu wa daraja la pili la poiti nane.
“Baada ya kufaulu nimechaguliwa kuendelea na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Liamungo iliyopo mkoani Kilimanjaro na familia yangu haina uwezo wa kunisomesha wala kunisaidia kwa chochote, naiomba Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan wanisaidie, pia wadau mbalimbali wajitokeze kunisaidia nikamilishe ndoto zangu za masomo,” amesema Haji.
Amesema licha ya changamoto za kimaisha anazokutana nazo, pia ana uwezo wa kuchora picha mbalimbali kwa kutumia miguu yake.
Anasema alipokuwa shule ya msingi, mwalimu wake aligundua kipaji alichonacho na kumsaidia kukikuza na sasa ana uwezo wa kuchora vizuri.
Caroline Mwanda, bibi yake Haji, amesema hana uwezo wa kufanya kazi kutokana na matatizo ya kiafya pamoja na umri mkubwa, hivyo anaiomba jamii imsaidie mjukuu wake.
“Kwa sasa sina uwezo wa kufanya kazi kulima. Niliacha muda mrefu. Kazi yangu ni kuchota maji ya kuoga na kula. Siwezi kushika jembe, nikidondoka na jembe shambani itakuwa nimejitakia mapigo ya moyo yanaenda kasi. Madaktari wamesema ni presha. Mjukuu wangu mmoja ameenda kufanya kazi za ndani kwa watu ili atusaidie. Namuomba Mama (Rais) Samia Suluhu Hassan amsaidie mjukuu wangu, siyo kwamba anapenda kuomba, ila hatuna uwezo,” amesema Mwanda.
Mwananchi Digital ilipata nafasi pia ya kuzungumza na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Kata ya Mtimbira, Henry Mwangake ambaye amesema anamfahamu mwanafunzi huyo. Amesema alipokuwa katika utekelezaji wa majukumu ya kikazi, alikutana na familia ya Haji na kugundua kuwa kijana huyo ana ulemavu wa viungo na pia anaishi kwenye familia isiyo na uwezo wa kifedha.
Hivyo amewaomba Watanzania kumchangia fedha kijana huyo aweze kujikimu mahitaji yake pamoja na kujiendeleza kimasomo.
“Nilipokutana na familia ya Haji na kuwahoji, licha ya kijana huyu kuwa na ulemavu wa viungo, niligundua kuwa familia hiyo haina uwezo wa kifedha na pia kuna mwanafunzi ambaye amekatisha masomo yake ili kuisaidia familia yake.”
“Niwaombe Watanzania kwa ujumla kujitokeza na kumchangia ili aweze kuendelea na masomo na pia apate angalau hela ya kujikimu kimaisha,” amesema mkaguzi Mwangake.