Mbowe, Lissu watakavyoongoza maandamano ya amani Chadema

Dar es Salaam. Ikiwa zimepita siku 54 baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kufanya maandamano ya amani katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha, imeandaa mengine ya nchi nzima.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti -Bara, Tundu Lissu watashiriki maandamano hayo na ratiba imetolewa ikieleza namna watakavyoyaongoza.

Kwa mujibu wa Chadema, maandamano hayo yanalenga kufikisha kilio cha wananchi kuhusu ugumu wa maisha, kusisitiza madai ya Katiba mpya na  kupata Tume Huru ya Uchaguzi ambayo imeanza kutumika pamoja na kupaza sauti ya namna gani nchi inaweza kukabiliana na majanga, yakiwamo ya mafuriko.

Viongozi waandamizi wa Chadema Taifa wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe leo wameongoza wafuasi wa chama hicho katika maandamano ya kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni, yaliofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba 

Katika awamu ya kwanza, Chadema ilifanya maandamano ya amani Januari 24, 2024 mkoani Dar es Salaam, Mwanza (Februari 16), Mbeya (Februari 20) na  Arusha (Februari 27).

Maandamano ya sasa ni matokeo ya Azimio la Mtwara lililofikiwa katika mkutano wa Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Machi mwaka huu mkoani Mtwara na kuazimia yafanyike mikoa yote nchini kuanzia Aprili 22 hadi Aprili 30, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Aprili 18, 2024 kuhusu maandalizi ya maandamano hayo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema baada ya tangazo la Azimio la Mtwara, maandalizi yanaendelea kufanyika.

Mrema amesema baada ya kufanya tathimini ya mambo mbalimbali ikiwamo hali ya hewa ya mvua wameamua kuyagawa maandamano kwa awamu mbili.

Amesema awamu ya kwanza itakuwa Kanda ya Serengeti inayohusisha mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu; Kanda ya Victoria yenye mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza.

Awamu ya pili amesema itahusisha Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha, Tanga, Manyara na Kilimnajaro; na Kanda ya Kati yenye mikoa ya Singida, Dodoma na Morogoro.

Amesema Aprili 22, Mbowe ataongoza maandamano Bukoba mkoani Kagera.

Aprili 23, ataenda Shinyanga na kuongoza maandamano yatakayofanyika Kahama, Aprili 24 atakuwa mjini Geita na Aprili 25 atakuwa Bariadi, mkoani Shinyanga.

“Aprili 26 atakuwa mjini Musoma na Aprili 27, ataenda Mwanza kuongoza maandamano yatakayofanyika wilayani Sengerema,” amesema.

Aprili 28, atakuwa safarini kuelekea Kaskazini ambako Aprili 29 ataongoza maandamano Tanga na Aprili 30 atahitimisha mkoani Kilimanjaro.

Kuhusu Lissu, amesema ataanzia Kanda ya Kaskazini kwa kuongoza maandanamo Aprili 25 mkoani Arusha.

Mrema amesema Aprili 26 ataenda Manyara, Aprili 27 atakuwa mjini Singida.

“Aprili 28 atakuwa safarini kuelekea Dodoma ambako Aprili 29 ataongoza maandamano mjini Dodoma na atahitimisha Aprili 30 mkoani Morogoro,” amesema.

Mrema amesema wameshalijulisha Jeshi la Polisi kwa kuwapelekea barua katika mikoa ambayo maandamano yatafanyika na njia yatakakopita.

Amesema ana imani polisi watawalinda kama walivyofanya katika maandamano ya Januari na Februari, mwaka huu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime, alipoulizwa na Mwananchi Digital iwapo wamepokea barua kutoka Chadema alitaka kujua ni mikoa gani maandamano hayo yamepangwa kufanya kwa kumtaka mwandishi kumwandikia ujumbe (sms) na baada ya kufanya hivyo ujumbe huo bado haujajibiwa.

Related Posts