DKT.DIMWA : ATAJA KIPAUMBELE CHA CCM

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na wanachama wa CCM wa Shina namba 12 Jimbo la Chumbuni Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na wanachama na wananchi kwa ujumla katika Tawi la CCM Masumbani Unguja.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akimkabidhi kadi mwanachama mpya katika Tawi la CCM Mgandini Jimbo la Shauri Moyo.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akipandisha bendera katika shina la CCM namba 10 Tawi la CCM Chumbuni.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amesema kipaumbele cha Chama Cha Mapinduzi ni kuzisimamia kikamilifu Serikali zake zitekeleze kwa vitendo maendeleo kwa maslahi ya Wananchi wote.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla katika mwendelezo wa ziara yake na Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC CCM Taifa Zanzibar katika Tawi la CCM Mkoa wa Mjini Wilaya ya Amani Unguja.

Dkt.Dimwa,alisema Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein  Mwinyi, imeendelea kutekeleza kwa ufanisi mambo mbalimbali ya maendeleo katika sekta za kiuchumi,kijamii na kimaendeleo.

Katika maelezo yake Dkt.Dimwa,alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhai wa CCM kwa kuzungumza na wanachama na kukagua miradi mbalimbali ya CCM na Jumuiya zake inayotekelezwa katika ngazi za Mashina,Matawi hadi Wilaya.

“Natumia nafasi hii kuwapongeza Wanachama na Viongozi wa ngazi mbalimbali za Chama na Jumuiya zake kwa kazi  nzuri za kuimarisha Chama chetu.
Tutaendelea kuhakikisha mambo yaliyoahidiwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita tunayatekeleza kwa ufanisi ili kutimiza dhamira Kuu ya Chama chetu ya kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha bora na yenye bora bila kujali tofauti za kisiasa,kidini na kikabila.

Alisema CCM imeendelea kuwa Chama bora nchini na barani Afrika kutokana na kujenga misingi imara ya Uongozi na Itikadi kuanzia ngazi za chini za Mashina utamaduni ambao haupatikani katika Vyama vingine vya kisiasa.

Aliwasisitiza Viongozi wa ngazi za Mashina na Matawi kufanya vikao vya kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 ili kupata nafasi ya kujadili,kutathimini na kufikia maamuzi ya pamoja ya kuimarisha Chama na Serikali zake.

Alitoa wito kwa Viongozi wa Mashina na kuwakumbusha wajibu wao ulioelekezwa katika Katiba ya CCM kuwa ni pamoja na kuongoza na kusimamia utekelezaji wa maamuzi yote ya CCM na utendaji wa kazi katika shina pamoja na kuhimiza ulipaji wa ada za Wanachama.

Aliyataja maelekezo mengine kwa Mabalozi hao wa Mashina kuwa wanatakiwa kulinda na kuendeleza siasa za CCM katika Mashina.

Dkt.Dimwa,alisema kazi nyingine ya Mabalozi hao ni kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao,kueneza Itikadi na siasa ya CCM katika Mashina pamoja na kuendeleza masuala ya maendeleo katika maeneo yao.

Pamoja na hayo,aliwataka Viongozi wa CCM wa ngazi za majimbo kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 ili Wananchi waridhike na sera za Chama na kukipatia ushindi katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kupitia ziara hiyo alisisitiza Wanachama hao kulipa ada kwa wakati ili fedha hizo zisaidie katika masuala ya kiutendaji na fungu lingine linarudi kwa mabalozi.

 Naye Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim  Kirupi,aliwasihi Wanachama wote wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa awamu ya pili ili kupata idadi ya mtaji wa kisiasa wa CCM.

Kilupi, aliwambia Wanachama hao kuwa muda wa Uchaguzi Mkuu unakaribia hivyo kila mwanacha ajipange kuhakikisha CCM inashinda ili iendelee kuongoza dola.

Kwa upande wa wananchi wa Wilaya ya Amani kwa wakati tofauti waliwapongeza viongozi wa Sekretarieti hiyo ya CCM Zanzibar kufanya ziara hiyo ambayo kwa upande wao imeacha matokeo chanya ya uimarishaji wa Chama.

Naye Khamis Farid Abdulla, Mkaazi wa Jimbo la Shaurimoyo, alisema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na uzinduzi wa miradi ya maendeleo  pamoja na nasaha mbalimbali za kuhamasisha wanachama na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkaazi wa Jimbo la Amani  Zuwena Mahmoud Issa, alisema ziara za aina hiyo zifanyike mara kwa mara kwani viongozi wengi wa ngazi za juu hawafiki katika matawi kusikiliza changamoto za wanachama hali  inayopelekea baadhi ya wanachama kukata tamaa.

Ziara hiyo katika Wilaya ya Amani ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Dkt.Dimwa imejumuisha Wakuu wa Idara za CCM na kutembelea,kukagua, na kushiriki ujenzi wa taifa katika miradi ya maendeleo katika mashina,matawi,wadi na majimbo yote ya wilaya hiyo .

Related Posts