KESI YA UKAHABA: Upande wa mashtaka kikaangoni kudharau amri ya mahakama

Dar es Salaam. Sakata la uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya ukahaba limechukua sura mpya, baada ya kujitenga na wajibu wake wa kutekeleza amri ya Mahakama inayoutaka kuwasilisha mahakamani taarifa ya kitabibu.

Jaribio la kujiondoa katika wajibu huo, baada ya kushindwa kutekeleza amri ya mahakama mara tatu limeshindikana kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive kutokubali utetezi uliowasilishwa.

Mahakama imesema upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha uthibitisho huo kama ulivyoelekezwa ni kupuuza amri ya mahakama, kwa kuwa wao ndio wanaomwakilisha shahidi, hivyo imepanga kutoa uamuzi kuhusu kupuuzwa amri hiyo.

Leo Jumatano Julai 3, 2024 baada ya kesi kuitwa, upande wa mashtaka umeieleza mahakama una shahidi mmoja na uko tayari kuendelea.

Hakimu Mfawidhi Lugano Kasebele anayesikiliza kesi hiyo, kabla ya kuendelea amehoji kuhusu utekelezaji wa amri aliyoitoa jana Julai 2, 2024 wa kuwasilishwa vyeti vya matibabu ya shahidi Konstebo wa Polisi Masadi.

“Jana tulisema kabla ya kuanza kesi tunataka taarifa ya matibabu ya Masadi (shahidi aliyedaiwa kuwa alikuwa mgonjwa), iko wapi?” amehoji Hakimu Kasebele.

Wakili wa Serikali, Mwasiti Ally amesema hawana taarifa na kwamba, kwa kuwa shahidi alifika mahakamani jana akatoa ushahidi basi kama ni taarifa yeye ndiye alipaswa kuitoa na si wao waendesha mashtaka.

Kwa majibu hayo, Hakimu Kasebele amewakumbusha wao ndio wanaomwakilisha shahidi huyo, akisisitiza amri za mahakama zikitolewa zinapaswa kutekelezwa.

Kutokana na amri ya mahakama kutotekelezwa, Hakimu Kasebele ameahirisha kesi kwa ajili ya kwenda kuandika uamuzi kuhusu kupuuzwa amri ya mahakama, ambao atautoa Jumatatu Julai 8, 2024.

Shahidi huyo, polisi wa kike Konstebo Masadi Madenge wa Kituo cha Polisi Magomeni Usalama, lilianza Alhamisi Juni 27, 2024.

Siku hiyo waendesha mashtaka mawakili wa Serikali, Tumaini Mafuru na Winfrida Ouko waliieleza mahakama walikuwa na mashahidi wawili lakini baada ya shahidi wa kwanza kwa siku hiyo kumaliza ushahidi, walisema wa pili waliyekuwa wamemuandaa amepata matatizo ya kiafya.

Kutokana na hilo, waliiomba mahakama itoe ahirisho aende hospitali kwa matibabu. Mahakama iliridhia.

Ijumaa Juni 28, 2024, waendesha mashtaka waliieleza mahakama walikuwa na shahidi mmoja lakini hali yake bado si nzuri, akitarajia kwenda hospitalini asubuhi.

Hakimu Kasebele alielekeza aitwe na alifikishwa mbele ya mahakama, akitembea kwa tabu akiwa ameshikiliwa na mmoja wa mawakili wa Serikali, akionyesha kukunja uso ishara ya kuugulia maumivu.

Baada ya mahakama kumuona waendesha mashtaka waliomba itoe ahirisho ili aende hospitali kwa matibabu.

Maelezo ya upande wa mashtaka kuhusu ugonjwa wa shahidi yalipingwa na mawakili wa utetezi, Peter Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi.

Madeleka alidai mahakama haina uwezo wa kubaini ugonjwa kwa macho badala yake akata upande wa mashtaka uwasilishe ushahidi wa vyeti vya matibabu.

“Jana tulielezwa shahidi ni mgonjwa anataka kwenda hospitalini tukaahirisha kesi. Kwa hiyo tulitarajia shahidi angeleta vyeti vya ugonjwa lakini na leo tena tunaahirisha kesi sababu ya shahidi kuwa mgonjwa na hakuna vyeti kithibitisha,” alipinga Madeleka.

“Shahidi waliyemleta leo siyo mgonjwa kwa maoni yetu, isipokuwa kama tutapata uthibitisho kutoka kwenye taasisi yenye mamlaka,” alisema.

Wakili Mafuru alikiri waliieleza mahakama kuwa shahidi ameugua na amekwenda hospitalini lakini siku hiyo (Ijumaa) walipomuita hakuwa na vyeti vya matibabu.

Alieleza shahidi alikuwa na dawa nyumbani ndizo alizotumia na siku hiyo ndiyo alipanga kwenda hospitali.

“Lakini tuliheshimu amri yako (hakimu) tumemuita aje hapa mahakama imuone, hivyo tunaomba mahakama impe nafasi ya kwenda hospitali maana anasema bado hajajisikia vizuri,” alisema wakili Mafuru.

Hakimu Kasebele katika uamuzi alikubaliana na hoja za mawakili wa utetezi.

Alisema Alhamisi kesi iliahirishwa shahidi akatibiwe, hivyo Ijumaa ilitarajiwa kutolewa uthibitisho wa taarifa ya matibabu.

“Kwa hiyo huyu (shahidi) anatumwa atuletee vyeti vya matibabu, kwa kumwangalia tu haitoshelezi, sasa waende hospitali watuletee vyeti,” aliagiza Hakimu Kasebele.

Alisema kama maelekezo hayo hayatatekelezwa mahakama itaona upande wa mashtaka umeshindwa kutimiza wajibu wake na itaweza kutoa uamuzi. Hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Jumanne Julai 2, 2024.

Jana kesi hiyo ilipoitwa upande wa mashtaka uliowakilishwa na mawakili wa Serikali Ouko na Cuthbert Mbilinyi uliieleza mahakama walikuwa na mashahidi wawili akiwemo shahidi huyo aliyekuwa anaumwa Konstebo Masadi.

Hata hivyo, hawakuwa na uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi huyo kama mahakama ilivyokuwa imeelekeza jambo ambalo liliibua mvutano.

Waendesha mashtaka waliomba kama vyeti hivyo ni muhimu basi kesi iahirishwe waende kuvitafuta.

Upande wa utetezi ulipinga hoja ya ahirisho badala yake ukaomba kesi iendeleee lakini mahakama ichukue hatua kwa upande wa mashtaka kwa kupuuza amri ya mahakama.

Akitoa uamuzi baada ya shahidi kumaliza kutoka ushahidi, Hakimu Kasebele alisema kitendo cha upande wa mashtaka kushindwa kuwalisha uthibitisho si sahihi na hakijamfurahisha kwa kuwa inaonyesha kupuuza amri ya mahakama.

Alisema hakuna ubishi kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha uthibitisho huo na hata shahidi amekamilisha ushahidi lakini hakuwasilisha vyeti vya matibabu.

Alisema Mahakama lazima iheshimiwe kwa mujibu wa Katiba na mtu yeyote bila kujali umri wake wala hadhi yake.

“Kwa leo Mahakama inawaonya jambo hili lisirudie lakini bado ninaomba taarifa ya Masadi kesho ije kwamba alikwenda hospitali na amri za mahakama ziheshimiwe,” alisema.

Kwa kutowasilishwa taarifa hilo leo Julai 3, Hakimu Kasebele amepanga kutoa uamuzi Jumatatu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mariam Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo, na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume cha kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.

Related Posts