UONGOZI wa klabu ya Simba umempa mkataba wa miaka miwili aliyekuwa kocha msaidizi wa Raja Casablanca, Fadlu David anayeelezwa atatua nchini Ijumaa sambamba na wasaidizi wake.
Kocha huyo ambaye amethibitisha ujio wake Tanzania baada ya kutumia ukurasa wake mtandao wa kijamii ‘Instagram’ kuwaaga viongozi, wachezaji na mashabiki wa timu aliyokuwa akiifundisha.
“Ulikuwa ni wakati mzuri, msimu mzuri, wachezaji bora, wafanyakazi wenzangu tulikuwa na benchi bora bila kuwasahau mashabiki.” Ni ujumbe wa kocha huyo akiwaaga.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti kuwa kocha hiyo anakuja na wasaidizi wake sambamba na meneja wa timu hiyo.
“Ni kweli Simba tulikuwa kwenye mazungumzo na makocha wawili akiwemo Msauzi, Steve Khomphela ambaye tumeshindwana katika baadhi ya mambo na kuamua kumalizana na David, ambaye amesaini miaka miwili,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Makubaliano na David ni kuja na wasaidizi wake ambao amewapendekeza mwenyewe watatua nchini Ijumaa kwa ajili ya kukamilisha mipango yote na baadaye timu kutimkia Misri tayari kwa maandalizi ya msimu mpya.”
Wakati ujio wa kocha huo mwenye Leseni A ya Caf na wasaidizi wake ukitarajiwa kuwasili nchini imethibitishwa kuwa kwenye benchi la ufundi la timu hiyo mchezaji wa zamani wa timu hiyo na kocha wa muda mrefu, Suleiman Matola ataendelea kuwepo huku ishu ya kocha Juma Mgunda ikiwa bado haijafamika.
“Mgunda alimaliza mkataba hajasaini mwingine na wala hayupo kwenye safari ya Misri Jumatatu.”