Raia kote nchini Uingereza watapiga kura zao kuanzia saa moja asubuhi siku ya Alhamisi, huku uchunguzi wa maoni ukibashiri chama cha Labour kitashinda uchaguzi wake mkuu wa kwanza tangu 2005, na kumfanya kiongozi wake Keir Starmer kuwa waziri mkuu mpya.
Matokeo hayo yatashuhudia Uingereza ikirudi kwenye mrengo wa wastani wa kushoto baada ya karibu muongo mmoja na nusu wa serikali za mrengo wa kulia za chama cha Conservative.
Soma pia: Chama cha Labour chazindua ilani kuelekea uchaguzi Uingereza
Starmer amekuwa akiizunguka Uingereza siku nzima ya leo, kwa kufika England, Scotland an Wales katika juhudi za kuimarisha uungaji mkono wa chama cha Labour na kuonya dhidi ya uridhikaji wa kizembe katika saa za mwisho za kampeni.
“Ikiwa unataka mabadiliko, unapaswa kuyapigia kura,” alisema Starmer mwenye umri wa miaka 61 wakati akizungumza na waandishi habari, na kuongeza kuwa hachukulii chochote kuwa jambo la kawaida.
Wahafidhina wamekuwa wakicheza na hofu ya watu, wakionya juu ya kupandishwa kwa kodi na kudorora kwa usalama wa taifa endapo wataondolewa mamlakani, katika kile chama Labour kimeelezea kuwa hatua za mwisho za ukataji tamaa kujaribu kusalia madarakani.
Pia wamezidi kuwahimiza wapiga kura katika wiki za hivi karibuni kuzuwia uwezekano wa chama cha Labour kushinda “wingi uliyopitiliza” — madai ambayo Labour inahofia yanakusudia kuathiri kiwango cha ushiriki wa uchaguzi huo.
Soma pia:Sunak na Starmer wakabiliana katika mdahalo wa mwisho kabla ya uchaguzi Uingereza
Waziri wa Kazi na Pensheni Mel Stride, mmoja wa washirika wa karibu wa Sunak, alisema leo kuwa wapiga kura “watajuta” kuwapa Labour mamlaka “isiyo na kipimo” bila upinzani imara wa Wahafidhina.
“Ukiangalia uchaguzi, ni wazi kwamba Labour katika hatua hii wanaelekea kwenye ushindi wa kiwango ambacho pengine hakijawahi kuonekana katika nchi hii hapo awali,” alikiambia kituo cha utangazaji cha mrengo wa kulia cha GB News.
Johnson: Siyo muda wa kukata tamaa!
Labour imefurahia uongozi thabiti wa alama 20 katika kura za maoni kwa muda wa miaka miwili iliyopita huku wapiga kura wengi wakielezea kutoridhishwa na namna chama cha Conservative kinashughulikia masuala mbalimbali yakiwemo gharama ya maisha, huduma za umma, uhamiaji na uchumi.
Soma pia: Rishi Sunak aitisha uchaguzi mkuu Uingereza
Lakini waziri mkuu wa zamani, Borris Johnson, aliyeondolewa madarakani na wenzake, akiwemo Sunak mwaka wa 2022 baada ya msururu wa kashfa, na ambaye hakuwepo kwenye kampeni muda wote, aliwataka wafuasi wa Conservative kutokata tamaa bado.
”Na kwa hivyo hakuna hata mmoja wetu anayeweza kukaa nyuma huku serikali ya Labour ikijiandaa kutumia wingi wa nyundo kuharibu mengi tuliyofanikisha, yale mlifofanikisha.”
Kinara huyo wa Brexit aliuambia mkutano wa hadhara Jumanne jioni kwamba Starmer atajaribu kuanzisha serikali ya mrengo wa kushoto zaidi ya Labour tangu vita vikuu vya pili vya dunia.
Mapema, kampuni ya uchunguzi wa maoni ya Survation ilibashiri kuwa Labour iko njiani kushinda zaidi ya viti 418 ilivyoshinda wakati Tony Blair alipohitimisha miaka 18 ya utawala wa Conservative mwaka 1997.
Chama hicho kinahitaji viti visivyopungua 326 kujipatia wingi wa kutosha kuunda serikali.