TARI YAHIMIZA WADAU KUTEMBELEA BANDA LAO SABAASABA KUJIFUNZA TEKNOLOJIA ZA KILIMO

Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wametoa wito kwa wadau mbalimbali wa kilimo na biashara kutumia fursa ya Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba) kutembelea Banda lao ili kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo kuanzia afya ya udongo hadi uongezaji thamani wa mazao.

Wito huo umetolewa na watafiti kutoka TARI, ambao wapo katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, yenye Kaulimbiu ‘Tanzania:Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji.’ TARI ikiwa inapatikana katika hema la Wizara ya Kilimo lijulikanalo kama hema la Katavi.

Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti TARI Kihinga, Dkt. Filson Kagimbo amesema, TARI imegundua Teknolojia mbalimbali zenye kujibu changamoto za wakulima ikiwa ni pamoja na ugunduzi wa mbegu za mavuno mengi zenye kuzaa mapema zikiwa na ukinzani wa magonjwa na stahimilivu na ukame ambazo elimu yake inatolewa katika maonesho hayo.

Pia elimu kuhusu usindikaji na upatikanaji wa masoko za bidhaa mbalimbali za kilimo ni miongoni mwa elimu ambazo zinatolewa na watafiti hao.

Naye, Mratibu wa usambazaji Teknolojia kituo cha Mikocheni, Kituo kinachofanya Utafiti wa Minazi kitaifa, Bi. Vidah Mahava amesema kupitia maonesho haya mkulima na wadau wengine wa Kilimo na Biashara wanapata fursa ya kujifunza teknolojia nyingi kutoka vituo mbalimbali kwa muda mfupi.

Charles Mwakalinga- Mkulima Mwekezaji wa matunda katika Mkoa wa Iringa na Dodoma ameeleza kufurahishwa na Banda la TARI ambalo anasema watafiti wameleta teknolojia ambazo kama mkulima amejifunza na anatarajia kuongeza tija kutokana na elimu aliyopata.

Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti TARI Kihinga, Dkt. Filson Kagimbo

Related Posts