MABOSI wa Tabora United wameanza mazungumzo na aliyekuwa kocha mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza kwa ajili ya msimu ujao.
Taarifa kutoka ndani ya kikosi hicho zinasema viongozi wamefungua mazungumzo na Baraza ili kukabidhiwa timu ikiwa ni muda mfupi tangu alipotemwa Dodoma Jiji na nafasi yake kuchukuliwa na Mecky Maxime.
“Ni kweli mazungumzo hayo yapo na ikiwa tutafikia makubaliano naye, atakuwa ndiye Kocha Mkuu wa Tabora United kwa ajili ya msimu ujao, kuanzia wiki hii tutaanza kujua mwelekeo mzima kuhusu suala hili,” alisema mmoja wa kiongozi wa Tabora.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Tabora United, Richard Abwao alisema, kwa sasa wao kama viongozi wana mambo mengi kwanza ya kufanya, ikiwemo kuhakikisha wanalipa fedha wanazodaiwa FIFA ili wafunguliwe kwa ajili ya usajili msimu ujao.
“Lengo letu la kwanza lilikuwa kuhakikisha kwanza timu inabaki Ligi Kuu Bara na tunashukuru tumefanikiwa kwa hilo, kwa sasa tunapambana na madeni tunayodaiwa na FIFA, kisha baada ya hapo ndipo tutaanza kuzungumza mambo mengine,” alisema.
Kwa upande wa Baraza alisema, taarifa hizo na yeye anazisikia ingawa kwa sasa yupo kwao Kenya kwa ajili ya mapumziko na ikiwa kutatokea jambo lolote ataliweka wazi, ingawa amekiri ni kweli kuna ofa mbalimbali hapa nchini ambazo amezipokea.
Mbali na kuifundisha Dodoma Jiji, pia Baraza amezifundisha timu mbalimbali nchini zikiwemo Biashara United na Kagera Sugar.