Shahidi amtambua jaji kama mtuhumiwa wa mauaji

Geita. Katika hali isiyotarajiwa, shahidi wa tatu kwenye kesi inayomkabili Zephania Ndalawa anayeshtakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia, amemtambua Jaji Graffin Mwakapeje kama mtuhumiwa wa mauaji ya Thomas Masumbuko.

Shahidi huyo, Salome Cheyo (9) akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Musa Mlawa alipotakiwa kwenda kumuonyesha mtuhumiwa kama anamkumbuka, alitoka kizimbani na kwenda hadi alipo jaji na kumuonyesha kuwa ndiye.

Hata aliposhuka kutoka alipo jaji na kurudi kizimbani na Wakili Mlawa kumuuliza tena kuhusu mtu mweupe aliyemfukuza siku ya tukio, mtoto huyo aliendelea kusisitiza ni jaji anayeendesha kesi hiyo, jambo lililozua vicheko mahakamani hapo.

Shahidi huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Burigi, alikuwa anatoa ushaidi wa tukio la mauji ya Thomas Masumbuko (12), jana Alhamisi Julai 3, 2024.

Masumbuko aliuawa kwa kufungwa kamba mguuni, mikono na kusokomezwa matambara mdomoni, hivyo kukosa hewa na kufariki dunia, huku akiwa amefunikwa kitambaa usoni.

Shahidi huyo akiwa kizimbani, Jaji alimhoji maswali ya ufahamu ili aweze kuapishwa, ikiwa ni pamoja na kumuuliza majina, dini na kama anajua nini maana ya dhambi au ukweli, maswali ambayo alishindwa kuyajibu kwa ufasaha.

Kutokana na kushindwa kujieleza, nini maana ya uongo au ukweli, Mahakama iliridhia shahidi huyo achukuliwe ushahidi wake bila kiapo.

Akitoa ushahidi huo, aliieleza Mahakama kuwa Agosti 19, 2023 akitoka kisimani kuchota maji, alikutana na pikipiki yenye watu wawili na mmoja alishuka na kuanza kumkimbiza na kumnyang’anya ndoo, kisha akamshika mkono na kumpeleka nyumbani anakoishi na bibi yake.

“Alipokuwa ananiingiza ndani, nilimng’ata mkono nikakimbia na kuingia kwenye nyumba ya mjomba ambayo iko pembeni na kwa bibi. Nilipofika, nilikuta mjomba amefungwa mikono na miguu anatoka damu kichwani,” alidai mtoto huyo.

Alidai baada ya kuona tukio hilo, alitoka na kukimbilia shambani alikokuwa shangazi yake na kumweleza kuwa nyumbani wamevamiwa na wameibiwa.

“Shangazi alikuwa na mume wake, walitoka mbio kuja nyumbani na kumkuta mjomba bado amefungwa anatoka damu,” alieleza Salome.

Alisesema Shangazi yake akiwa bado kwenye nyumba ya mjomba huyo, yeye alitoka na kuingia kwenye nyumba ya bibi yake kuchukua maji, ndipo alipomkuta Thomas Masumbuko (marehemu), amefungwa mikono na miguu na usoni alikuwa amefungwa kitambaa.

Akiongozwa na Wakili Mlawa, aliulizwa kama anatambua wajihi wa mshtakiwa, alidai ni mweupe mrefu kiasi na ni mtu anayewabebea mazao shambani wakati wa mavuno.

Wakili Mlawa alimtaka kwenda kumwonyesha mtuhumiwa kama yupo mahakamani, ndipo alipokwenda kumuonyesha jaji anayesikiliza kesi hiyo.

Akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa utetezi, Beatrice Amos kama anamfahamu mshtakiwa aliyeko kizimbani, shahidi huyo alidai hamfahamu na kuhusu pikipiki ya mshtakiwa iliyoko kwenye chumba cha mahakama, alidai pia haitambui.

Shahidi mwingine Leticia Herman (33) ambaye ni mama mzazi wa Thomas Masumbuko (marehemu), ameieleza mahakama kuwa siku ya tukio Agosti 19, 2023, aliamka asubuhi saa moja kwenda shambani ilipofika saa nne walikuja watoto shambani wakikimbia wakidai nyumbani kumevamiwa.

“Nilitoka shambani na kwenda nyumbani, nikamkuta kaka yangu Lufungulo Nderema amefungwa mikono na miguu akiwa na majeraha ya kukatwa, huku akitoka damu nyingi kichwani na kwenye shavu,” alidai Hermani.

Alidai baada ya kumkuta kwenye hali hiyo akisaidiana na mume wake, walimfungua kamba na kitambaa usonim wakamtoa nje kumpa msaada, lakini kabla hawajamsaidia alikuja Salome akipiga kelele, akidai Thomas naye amefungwa vivyo hivyo kama mpwa wake.

Alidai baada ya kuingia kwenye nyumba nyingine alikokuwa, Thomas Masumbuko walimkuta amefungwa mikono na miguu na kufungwa na kitambaa cha shuka usoni, huku akiwa amewekewa nguo mdomoni hadi puani, ndipo alipoanza kupiga yowe majirani wakaja.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Deodatha Dotto alimtaka aeleze alichoelezwa na Salome pindi alipomfuata shambani na yeye (shahidi) akasema Salome alisema wamevamiwa  nyumbani.

Alipoulizwa kama alimwambia aliyesababisha mauaji hayo, shahidi huyo alidai hakuelezwa na alipoulizwa kama Salome alimuona mtu wa aina gani, alidai kijana mmoja ana rangi ya maji ya kunde mrefu kidogo.

Alipoulizwa kama anamtambua mshtakiwa alidai anamfahamu kwa kuwa ndiye anayemsaidia kubeba mazao shambani na alipoulizwa kuhusu kuhusika na mauaji, alidai hafahamu kwa kuwa wakati wa tukio hakuwepo.

Shahidi wa tano katika kesi hiyo, Petro Albert alieleza kuwa siku ya tukio Agosti 19, 2023 akiwa anauza matofali nyumbani kwake Msilale, walifika watoto wakikimbia wakidai nyumbani kwao kuna watu wamevamia na kuiba mahindi.

“Niliambatana na Salome hadi nyumbani kwao na niliona michirizi ya pikipiki na kumkuta mama Salome analia akidai wamemuua mtoto wake na kuiba mahindi na tulipoingia ndani tulimkuta Lufungulo Nderema amefungwa miguu, mikono na usoni huku akiwa amekatwa kichwani na alikua hajitambui,” amesema Albert.

Akiulizwa maswali na wakili wa utetezi kama watoto walimweleza kuhusu wauaji, alisemai hapana na kuhusu marehemu kama alinyongwa, shahidi huyo alidai alikuwa amefungwa kitambaa na kamba ilikua imekazwa sana shingoni na kulikuwa na vitambaa mdomoni na puani.

Kesi hiyo inaendelea asubuhi hii katika Mahakama Kuu masjala ndogo ya Geita kwa kusikiliza mashahidi wa upande wa mashtaka.

Related Posts