Vita vya kodi mtihani kwa vigogo TRA

Dar/Unguja. Kama ilivyoripotiwa kwenye gazeti hili kwamba, mgomo wa wafanyabiashara ulioanza Kariakoo, Dar es Salaam na baadaye kusambaa maeneo mengine nchini utawang’oa vigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hatimaye imetokea.

Juzi usiku, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko kwa kumuondoa aliyekuwa Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata na kumteua Yusuf Mwenda kushika wadhifa huo kwenye taasisi hiyo muhimu na nyeti kwa uchumi wa nchi.

Katika uteuzi huo, Rais Samia pia amewabadilisha mawaziri wawili – Dk Seleman Jafo ameenda kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, akibadilishana nafasi na Dk Ashantu Kijaji aliyekuwa Wizara ya Viwanda. Jafo awali alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira.

Juni 24, Mwananchi iliripoti habari kuhusu mgomo huo wa wafanyabiashara uliodumu kwa takribani siku nne kwamba ungewaondoa vigogo TRA.

Kidata, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Balozi wa Tanzania nchini Canada na Katibu Tawala, anaondoka TRA akiwa ameandika rekodi kwenye ukusanyaji mapato kwenye chombo hicho. Kidata ameteuliwa kuwa mshauri wa Rais, Ikulu.

Mrithi wake, Mwenda aliwahi kuwa Meya wa Manispaa wa Kinondoni, baadaye Naibu Kamishna ndani ya TRA, kisha akateuliwa kuwa Kamishna wa Mapato Zanzibar (ZRA), anarejea ndani ya mamlaka hiyo kuendeleza jahazi.

Mabadiliko hayo yamefanyika siku chache baada ya mgomo wa wafanyabiashara Kariakoo na baadaye mikoa mingine, ambao unatoa picha ya vita iliyopo na inayomsubiri Mwenda katika udhibiti wa ukusanyaji na ukwepaji wa kodi, na utendaji ndani ya mamlaka hiyo.

Mwananchi lililokuwa mstari wa mbele kuripoti taarifa za mgomo huo, lilizungumza na wadau kadhaa kutafuta kiini cha tatizo, ambao pamoja na mambo mengine walitaja sheria za kodi kuwa zinasababisha matatizo makubwa.

Serikali ilikutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara na kufikia makubaliano ya kumaliza mgomo huo kwa kuweka maazimio 15, ikiwamo TRA kusitisha kamatakamata na ufuatiliaji wa risiti za EFD katika maeno yote hadi Agosti, 2024.

TRA kwa upande wake, licha ya kutajwa kuwa wababe katika kusimamia sheria wakati wa kukusanya kodi, wanaelezwa pia ni wagumu kusikiliza changamoto za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara wakiamini ni wadanganyifu.

Mvutano kati ya TRA na wafanyabiashara wakubwa, ambao wamekuwa wakishirikiana na wale wa kati, umeshika kasi baada ya Serikali kutangaza kubadilisha utaratibu wa kukusanya kodi.

Mwenda atakabiliana na hali hiyo ambayo kwa sasa imepoa, huku baadhi ya madai ya wafanyabiashara yakiwa hayajapatiwa ufumbuzi wa kudumu, ikiwamo kamatakamata ya wafanyabiashara na wateja na wasiotoa au kuchukua risiti za kielektroniki (EFD), mtawalia.

Mtihani mwingine kwa Mwenda dhidi ya madai ya wafanyabiashara ni utitiri wa machinga mbele ya maduka ya wafanyabiashara wakubwa, ambao wanadai TRA imeshindwa kuwapatia ufumbuzi licha ya mikakati ya mara kwa mara ya Serikali kuwapangia maeneo maalumu ya biashara.

Pia, wafanyabiashara wanataka pendekezo la bei elekezi ya kuingiza kontena kulingana na bidhaa zinazoingizwa, badala ya kukadiria, utaratibu ambao wamedai ni kichocheo cha rushwa.

Utaratibu wa sasa wa wafanyabiasharam hasa wa Kariakoo, kununua bidhaa kutoka nje ya nchi – China, India, Dubai na Uturuki, kisha kusafirisha kwa makontena kwa pamoja, kupitia mawakala wa usafirishaji, umetajwa pia kuwa kiini cha mgogoro.

Mtindo huu huitwao consolidation (kuunganisha kodi ya forodha kwa pamoja), unatajwa kuongeza uwezo wa mizigo ya wafanyabiashara kufika nchini kwa haraka.

Hata hivyo, kuna changamoto kwenye utaratibu huo kwa kodi za forodha bandarini kwa kuwa ‘Bill of Landing’ (nyaraka za kuonyesha aina ya mzigo, ujazo wake na mahali unakopelekwa,”  huwa ni moja kwa mizigo yote iliyoingizwa pamoja, hivyo kodi kulipwa na msafirishaji aliyekusanya mizigo.

Kwa mujibu wa mmoja wa wafanyabiashara, TRA kupitia utaratibu huo, inaamini unapoteza mapato kwa sababu mwenye mzigo hukosa risiti ya kulipa ushuru wa forodha, ushuru wa bidhaa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

“Huu utaratibu umekuwa msaada kwetu, lakini TRA hawautaki na sasa wanataka utaratibu wa de-consolidation (kila mwagizaji kulipa mwenyewe ushuru) ili kila mwagizaji awe na hati yake ya kusafirisha na kulipia mizigo, badala ya kodi kulipwa na msafirishaji mmoja,” amesema mfanyabiashara huyo ambaye hakupenda kutajwa jina.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya TRA zinadai utaratibu huo umekuwa ukitumika kama mwanya kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kodi.

Imeelezwa wapo wafanyabiashara wakubwa wanamiliki maghala ya kuhifadhia mizigo, ambao hudai inapita kwenda nje ya nchi, hivyo kutolipiwa kodi, lakini baadaye huingizwa sokoni nchini.

“Watu hawataki kufuata sheria, wamenufaika sana kwa kukwepa kodi kupitia mfumo huu, wapo wanaofanya kwa uaminifu, ila wengine wanakwepa kodi. Unakuta ghala limejaa vitenge na unapohoji wanadai vinakwenda nje ya nchi, lakini baadaye huingizwa sokoni. Hata ukijaribu kufuatilia kwenye mipaka kwamba, kuna mizigo imepita huoni taarifa zake,” kimesema chanzo kimoja ndani ya mamlaka hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Rogers Lumenyela, mchumi kutoka Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Dodoma, amesema Mwenda ana kibarua cha kuongeza wigo wa walipakodi.

Dk Lumenyela amesema taarifa zilizopo zinaeleza walipakodi bado wachache wanaolipa moja kwa moja kwa TIN namba, akisema kundi jingine likilipa kwa njia ya kununua bidhaa.

“Ili kuongeza wigo, lazima kuwezesha na kuongeza sekta za uzalishaji, kibarua chake ni namna ya kuongeza wigo wa walipakodi, hatua itakayopunguza malalamiko ya watu wanaodai kuwa kodi na ushuru vipo juu,” amesema.

Kwa mtazamo kama huo, Mhadhiri Mwandamizi wa Biashara wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Felix Nandonde amesema Mwenda anatakiwa kuangalia namna bora ya kurasmisha biashara ndogondogo ili kuhakikisha wigo wa walipakodi unaongezeka.

Dk Nandonde amesema pia anakabiliwa na kibarua cha kutatua kilio cha muda mrefu cha wafanyabiashara kubambikiwa makosa ya kikodi.

Mfanyabiashara Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema jukumu la kwanza la Dk Jafo na Mwenda ni kupitia sheria zinazosababisha changamoto, akisema Rais Samia amekuwa akitoa maagizo kuhusu jambo fulani lakini matokeo yake halitekelezwi kwa ufasaha.

“Katika sekta zote, si biashara tu, mara kadhaa unasikia marufuku inatolewa lakini utekelezaji wake unasuasua. Ukirudi katika biashara, TRA inaagizwa isifanye hivi, lakini bado wanafanya,” amesema.

“Hii ni kwa sababu sheria inawaruhusu kufanya hivyo, kwa hiyo jukumu la kwanza ni kupitia sheria zinazoleta shida na kupelekwa bungeni zikabadilishwe, kumleta kamishna mpya wa TRA bila kumpa uwezo wa kisheria wa kusimamia, yatakuwa mambo yaleyale,” amesema Sugu ambaye pia ni mwanasiasa.

Sugu amedai mabadiliko ya watendaji hao yaliyofanywa na Rais Samia yametokana na malalamiko ya mabalozi waliomba kukutana na Serikali kujadili changamoto zinazowakabili wawekezaji wa kigeni.

Katika barua yao ya Juni 26, 2024  mabalozi waliomwandikia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba wakieleza kuwa, licha ya ongezeko la usajili wa biashara kutoka Dola bilioni 3 za Marekani mwaka 2022 hadi Dola 5.5, wawekezaji wanakumbana na vikwazo vikubwa kutoka TRA.

Mabalozi hao kutoka Uingereza, Marekani, Uholanzi, Ireland, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Sweden na Ujerumani walizungumzia pia ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa kwa kampuni za kigeni nchini.

Waziri Makamba alikubali ombi la kuonana nao kujadili changamoto walizoziwasilisha, akiwahakikishia kikao hicho kitakuwa na mawaziri wa sekta za fedha, mipango na uwekezaji, viwanda na biashara na kamishna wa TRA.

Mwenda aliwahi kuwa diwani wa Mikocheni na Meya wa Kinondoni kuanzia mwaka 2010/2015.

Wakati akihudumu wakati wa umeya alikuwa pia mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kitengo cha wateja wakubwa.

Machi mosi, 2022 Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi alimteua Mwenda kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), akichukua nafasi ya Salum Yussuf Ali aliyetenguliwa.

Desemba 29, 2022 katika kilele cha sherehe za mlipakodi, 2021/22, Dk Mwinyi alimpongeza Mwenda kwa kazi nzuri akisema ZRA imekuwa na mwelekeo mzuri katika ukusanyaji wa mapato tofauti na vipindi vilivyopita.

Wakati Mwenda anateuliwa kuongoza ZRA alikuta makusanyo kwa mwaka Zanzibar yakiwa Sh374 bilioni (mwaka 2021) na hadi Juni mwaka 2023/24 kufikia, imekusanya Sh718.7 bilioni ikivuka lengo la kukusanya Sh675.6 bilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 106.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenda Julai 2, 2024, siku aliyoteuliwa kuongoza TRA, ilieleza makusanyo yameongezeka kwa asilimia 27.01 sawa na Sh152.8 bilioni ikilinganishwa na mapato halisi ya mwaka wa fedha uliopita 2022/23 yaliyokuwa Sh565.8 bilioni.

Wakati Mwenda anashika nafasi hiyo, alibadilisha mtazamo na kuwaweka wafanyabiashara karibu na wafanyakazi wa mamlaka hiyo badala ya kuwaona kama maadui.

Tofauti na ilivyo kwa watendaji wengine, Mwenda alikuwa akitoka na timu yake kwenda katika maeneo mbalimbali kuzungumza na wafanyabiashara kusikiliza kero, huku akiwauliza ni namna gani wanaona utendaji wa ZRA na nini cha kufanya ili kubadilisha utendaji huo.

Alianzisha utaratibu wa kutembelea wafanyabiashara mmoja mmoja na makundi kuzungumza nao, kusikiliza kero zao, jambo lililowaweka wadau hao karibu na kuona hakuna sababu ya kuwakimbia watendaji wa ZRA.

Related Posts