Samia akitimiza hili, atakuwa Rais wa pili kuacha alama ya kudumu

“Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) angeandika historia ya kukumbukwa milele na Watanzania kama kwenye utawala wake atafanikisha upatikanaji wa Katiba Mpya,” ni kauli ya mwanasiasa James Lembeli katika mwendelezo wa mahojiano maalumu na Mwananchi.

Lembeli anasema, hiyo ingekuwa ni alama ya milele kwa Rais Samia na ndiye angekuwa mtu wa pili kuacha alama ya kukumbukwa milele, baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyeongoza mapambano ya kudai uhuru wa Tanganyika.

Akitolea mfano sasa, anasema vijana ambao walizaliwa baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere (Oktoba 14, 1999), leo hii wakisikia nukuu zake kwenye redio au televisheni, wanasikiliza, lakini hawakumuona akiwa hai.

“Unadhani ni kwa nini? Mwalimu alikuwa na maono; alivyovizungumza wakati ule ndivyo vinatokea sasa. Ni Rais ambaye anakumbukwa na Watanzania milele,” anasema Lembeli katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Julai Mosi, jijini Dar es Salaam, yakiangazia masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii.

Anasema Rais Samia pamoja na mambo mazuri anayoyafanya kwenye kipindi chake, ikiwamo kuanza kwa safari za usiku, kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ambayo, ingawa hayaridhishi, angalau yamefanyika, kama atakubali katiba mpya katika kipindi chake, ataandika historia ya kukumbukwa milele na isingesahaulika kwa vizazi na vizazi.

“Japo naye ni kama anapata shida ndani ya chama chake, kwani wanajua akiipitisha, chama nacho kitapata shida.

“Lakini katika siasa, ukiona mwenzako ananyolewa, zako tia maji kwa kuwa dunia inabadilika na mambo yanabadilika. Leo hii vyama vingi vikongwe Afrika ziko wapi? Hata kwa Watanzania napo ipo siku. Angalia Kenya, KANU ipo wapi? Afrika Kusini, Malawi, Zambia na nchi nyingine nyingi vyama kongwe vingi vimeshaanguka.

Anasema, hata hapa nchini, kwa kuwa ni nchi iliyo kwenye mfumo wa vyama vingi, ipo siku mambo yatabadilika, lakini alama anayoiacha kiongozi haifutiki.

Anasema, alama kubwa na ya pekee ambayo Rais Samia ataiacha ni kama katiba mpya itapatikana kipindi chake.

“Tunaambiwa hadi elimu itolewe. Elimu gani? Unampa nani? Ili iweje? Nchi hii sio ya kufanyia majaribio akili za watu. Tume ya Jaji Warioba (Joseph, waziri mkuu mstaafu na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba) ilifanya kazi ile kikamilifu kabisa, halafu leo unasema uendelee kutoa elimu kwa nani?

Anasema, mchakato wa mabadiliko ungeendelea pale ulipoishia kwa kuwa tume ilifanya kazi yake ipasavyo na ilitumia gharama kubwa kufanya ile kazi.

“Mimi naamini Mama (Rais Samia) anafanya kazi nzuri, japo mwanzo baada ya kifo cha Magufuli (John Pombe, Rais wa awamu ya tano), wengi hawakuamini kama ataweza kufanya haya anayoyafanya sasa.

“Ameweza na kikubwa ni kuendelea kumuombea na kuombea pia uchaguzi wa mwakani uwe wa amani,” anasema Lembeli na kusisitiza endapo atapata nafasi ya kumshauri Rais Samia, angemshauri kuwatumia wazee ili kupata taarifa nyingi za kweli.

Anasema, hivi sasa kuna vitu vingi vinaendelea, lakini ni kama Rais haambiwi ukweli, akitolea mfano changamoto za vituo vya afya na zahanati nyingi kuwa na changamoto za dawa.

“Utakuta huku nje tunaambiwa dawa zipo, lakini nyingi ukienda hakuna ila utaelekezwa ukanunue kwenye duka la ‘kigogo’. Wazee wanaambiwa matibabu bure, lakini ni vipimo tu, dawa hawapati. Kuna changamoto nyingi sana kwa wananchi,” amesema.

Lembeli anasema kingine ambacho kinaivuruga nchi ni uwepo wa uchawa, jambo ambalo anasema ni teminolojia (msamiati) mbaya sana na inaharibu vitu vingi.

“Ajabu kuna viongozi nao wanapenda na wanafurahia uchawa. Kwa hali ilivyo, Mama (Rais Samia) ana kazi ngumu sana. Kingine ni watu ambao wangeweza kusaidia kumshauri wameshaondolewa.

“Hao machawa wanahisi wale ambao wana profesheni zao, wenye uwezo mkubwa, wakiendelea kuwepo watawaharibia. Hivyo wanafanya fitina na mivurugano tu. Katika vitu ambavyo natamani visipewe uzito ni hawa wanaojiita machawa kujipenyeza penyeza kwa Mama.”

Hata hivyo, Machi 13, 2024, alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowachagua, Rais Samia aliweka msisitizo kwamba hana kundi na kuwakataa wale ‘machawa’ waliokuwa wakijiita wao ni wa Mama.

Christopher Lembeli, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kahama kwa miaka 10 kwa tiketi ya CCM kabla ya kuhamia upinzani mwaka 2015 na kurudi CCM mwaka 2016, anasema chama hicho tawala ni kizuri, ingawa hajui kinapotelea wapi.

“Ukiisoma Katiba ya CCM inasema ni chama cha wafanyakazi na wakulima, leo hii tujiulize ni chama cha wakulima na wafanyakazi kweli?” anahoji Lembeli.

“Kama sio hivyo, je? Waliopo ndani ya CCM wapo kwa niaba ya wakulima na wafanyakazi? Kama wapo, kwa nini wanaruhusu kikokotoo? Mafao ya mfanyakazi ni yake, kwa nini asimamiwe jinsi ya kuyatumia? Mbona huko nyuma haikuwa hivyo, mtu alipostaafu, nikiwemo mimi, nilipewa mafao yangu yote. Kwanini sasa wanapeleka kidogo (asilimia 40 kutoka 36)?”

“Kama ni chama cha wakulima, kwanini wanaruhusu wakulima waendelee kukopwa? Inafanya wengi waone ukulima hasa wa mazao ya biashara kama ni mateso. Kilimo cha pamba kanda ya ziwa, kahawa yakoje? Mazao mengi ya biashara ni kama yamekufa,” anasema.

Lembeli anasema Kahama, wengi wamegeukia uchimbaji wa madini ya dhahabu, ambako ndiko wanapata hela.

“Wachimbaji wadogo wadogo Magufuli aliwatengenezea mfumo mzuri, hawatapeliwi tena. Akipata dhahabu akaenda soko la madini, unaiuza vizuri,” anasema.

Lembeli, ambaye amekuwa Mbunge kwa miaka 10 katika kipindi chote cha utawala wa Rais Jakaya Kikwete, anasema wakati huo, watumishi wa Serikali hawakuwa na viburi.

“Leo hii ukienda vituo vya afya vingi ambavyo ndivyo vinahudumia watu wa chini, vina changamoto. Taasisi nyingi za Serikali zina shida, utekaji ulifutika lakini sasa ni kama unarudi. Tunaona kuna maeneo polisi wanaua watu, wananchi wanajibu.

“Haya mambo hapa katikati yalikwisha, lakini ni kama yanaanza kurudi tena. Kuna wakati unawaza wanaofanya labda wana nia ya kumharibia Mama!”

Anasema ni kama Rais anapata shida hasa kwa wanaompa taarifa. Akimgusia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, anasema Mwalimu alikuwa akijua taarifa zote.

“Ilikuwa huwezi kumdanganya. Nakumbuka nikiwa mdogo, Mwalimu alikuwa na utaratibu akifanya ziara mkoani, watu wa kwanza kuonana nao walikuwa ni wazee. Wazee huwa hawana cha kuficha, wala kujikomba, wanamwambia Rais ukweli. Watendaji wake mara nyingi walimuogopa, waliogopa kumwambia ukweli na wengine kusema vitu ambavyo waliona vitampendeza, lakini alipokuwa akikutana na wazee walimwambia ukweli na alikuwa na taarifa zote. Mwalimu ilikuwa humdanganyi,” anasema Lembeli.

Lembeli, ambaye kitaakuma ni mwandishi wa habari na mtaalamu wa masuala ya utalii, anasema mara zote hutoa ushauri kuhusu uhifadhi na utalii nchini na kimataifa kwa muda mrefu. Anasema kuna changamoto katika sekta hiyo nchini Tanzania.

“Uhifadhi ni sayansi kwa asilimia 100. Inapotokea taasisi ikaongozwa na mtu ambaye si mhifadhi, hapo ipo shida. Ni kama leo hii mkurugenzi wa Hospitali ya Muhimbili awe na taaluma ya uhasibu; mambo yatakwenda?” anahoji.

Anasema kuwa na kiongozi kwenye taasisi fulani ambaye hana ‘passion’ ya jambo analoliongoza ni tatizo.

Anatoa mfano wa uhifadhi na hali ilivyo sasa, ikiwemo miundombinu ya Serengeti ambayo anasema siyo mizuri.

“Niliwahi kusema kuhusu filamu ya Royal Tour (iliyofanywa na Rais Samia kwa ajili ya kuhamasisha utalii), watu wataiangalia hiyo filamu lakini wakienda hifadhini watakuta kuna tofauti.

“Filamu ya Royal Tour niliwahi kusema haina tofauti na ile ya ‘Serengeti Shall Never Die’ ilirekodiwa miaka 50 au 60 iliyopita, lakini hadi leo bado ina umuhimu ule ule? Sababu kuna miundombinu inayoifanya iendelee kudumu,” anasema.

Anasisitiza kuwa serikali inahitaji kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wenye uelewa, uzoefu, na mahaba na masuala ya uhifadhi na utalii. Bila ushauri huu, Royal Tour haitaweza kuendelea kudumu na kuleta manufaa kama ilivyokusudiwa.

Anashauri serikali kuwekeza katika miundombinu, kutoa motisha, na mambo mengine yanayoweza kuboresha zaidi eneo la uhifadhi na utalii.

“Ukiwapa walinzi wa hifadhi motisha, watafanya kazi kwa moyo. Haya masuala ya kuua tembo na faru na watu kufanya ujangili yatadhibiwa. Zamani askari ukienda porini ukamkata jangili au silaha unalipwa posho. Kama hazipo na hali ilivyo ngumu, ni rahisi jangili kumshawishi kwa pesa ili waingie kuua tembo.

“Kinachotokea ni askari anabadilisha lindo kwenda upande ambapo tembo hawapo kwa kuwa wanajua.”

Anasema wakati wa awamu ya tano, wahifadhi wenye taaluma walitolewa wengi, akitolea mfano pia Ngorongoro ambako anadai walioifahamu vyema wamesambaratishwa wote.

“Ndiyo maana tunaona pale pana shida na haiwezi kuisha. Tusipoangalia ile jamii ya pale ina mila na taratibu zao, ni watu maalumu. Wale watu ukitaka kufanya nao kazi lazima uzifahamu. Kwanza, Masai mzee hawezi kukaa na kujadili jambo na kijana mdogo; anaona kwamba umemdharau hata hawezi kukusikiliza. Ilipaswa wanaokwenda kule wawe wanafahamu mila zao.

“Leo hii unamtoa kijana amevaa mlegezo anakwenda kuongea na wale wazee, ni nini? Tulisikia waliwapiga watu kule. Hii ni migogoro ambayo kimsingi inasababishwa na kukosekana kwa watu ambao wana ushawishi wa kuzungumza na jamii ile.”

Anasema kuzungumza na mmasai hadi akuelewe inahitaji ujue mila na desturi zao. Anakumbuka moja ya tukio ambapo yeye, Lembeli, na aliyekuwa waziri Khamis Kagasheki walikwenda kutatua mgogoro makao makuu ya hifadhi hiyo.

“Aliposimama Kagasheki kuzungumza, wale wazee walimkataa, wakaomba mimi niongee kwa kuwa kwao wanaona ukiwa na mvi ni mtu mwenye hekima. Sababu tulijua, nilimwambia waziri wangu mapema, ikabidi mimi ndiyo nizungumze nao. Walifurahi na makofi walipiga; wale ni watu maalumu,” anasema.

Related Posts