“Waziri kaniambia ile Sheria ya Msajili wa Hazina tayari imeshakamilika na iko tayari kusomwa kwa mara ya pili bungeni. Kwa hiyo naomba wabunge nendeni kaijadilini, mnapoona hapako vizuri turekebisheni, lakini ile sheria ipite ili apate mwongozo wa kumwongoza huyu (Msajili wa Hazina).
“Lakini jingine, tuwe na uwezo sasa wa kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji. Tutakapoanzisha Mfuko wa Uwekezaji nchini, ndipo mashirika yetu haya ambayo yako asilimia 100 ya Serikali wanaweza kupata mtaji na kuendelea na kazi zao. Mtaji wenye usalama kabisa.”
Haya ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa jijini Dar es Salaam Juni 11, 2024 wakati akipokea gawio la Serikali kutoka kwa Mashirika ya Umma na Taasisi ambazo Serikali ina hisa kidogo.
Rais Samia, ambaye ni muumini wa mageuzi ya kiuchumi, alitoa kauli hiyo wakati akirejelea takwimu zilizotolewa siku hiyo wakati anapokea gawio la jumla ya Sh637.12 bilioni, ikijumuisha gawio la Sh278.86 bilioni kutoka katika mashirika ya biashara na michango Sh358.25 bilioni kutoka katika taasisi nyingine, yakiwa ni makusanyo kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Mei 2024.
Alisema hivyo huku akiyahimiza mashirika ambayo yana umiliki wa asilimia 100 wa Serikali, hasa yanayofanya biashara, yaongeze jitihada na ubunifu katika kuzalisha ili yalete tija kama yale ambayo Serikali ina hisa chache.
Si hivyo tu, pia alihimiza Bodi za Mashirika ya Umma ziwajibike na kuyasimamia mashirika hayo kwa weledi, ili hatimaye faida ya uwepo wa mashirika hayo ionekane.
Lakini pia akaridhia maombi ya Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, na Mwakilishi wa Wenyeviti wa Bodi za Mashirika ya Umma, Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali Venance Mabeyo, la kutaka Wajumbe wa Bodi za Mashirika ya Umma waombe na wafanyiwe usaili ili kuwezesha mashirika kupata wajumbe watakaoongeza tija katika usimamizi wa taasisi hizo.
“Wajumbe wa bodi watashindana kupata nafasi ya bodi. Ile mambo ya angalau hata bodi yasiwepo… mimi mtaniachia uteuzi wa wenyeviti, ili ziwe na watu ambao wanajua mambo yanayoendelea,” akasema.
Muswada wa Sheria Mpya ya Uwekezaji wa Umma ulisomwa Bungeni kwa mara ya kwanza Ijumaa, Novemba 10, 2023, na kupitishwa kwake kuwa Sheria siyo tu kutampa mamlaka Msajili wa Hazina wa kuyasimamia kwa tija, lakini pia utaondoa ukiritimba ambao mara nyingi unakwamisha ufanisi kwenye mashirika hayo.
Uwekezaji wa Serikali upo katika taasisi na mashirika takriban 298, ambapo kati ya hayo, 248 ni taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali ambapo zote ziko ndani ya nchi, na 50 ni kampuni ambazo Serikali ina hisa chache, kati yake 40 ziko ndani ya nchi na 10 ziko nje ya nchi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, taasisi, mashirika na wakala za Serikali 213 zinajihusisha na utoaji wa huduma, wakati 35 zinafanya biashara, wakati ambapo kampuni 50 zote ambazo Serikali ina hisa kidogo, zinajihusisha na biashara.
Serikali imefanya uwekezaji wa Sh73 trilioni katika taasisi, mashirika ya umma na Wakala za Serikali 298 zinazofanya shughuli mbalimbali.
Endapo Sheria hiyo itapitishwa, ni dhahiri kwamba, baada ya miaka mitano, baadhi ya mashariki yanakwenda kufanya vizuri, watendaji wa mashirika hayo watapimwa kwa ufanisi wa kazi ili kuhakikisha wanafikia malengo yaliyowekwa.
Vipengele vilivyomo kwenye Muswada huo ambao ukipitishwa utakuwa Sheria, vinawataka wakurugenzi wa mashirika ya umma kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha wanapata mafanikio katika utendaji wao.
Sheria hiyo inapaswa kuipa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, mamlaka ya kuidhinisha stahili za wajumbe wa bodi za taasisi, kwa sababu kwa sasa Msajili wa Hazina hana mamlaka ya kuidhinisha viwango vya stahili za wajumbe wa bodi, na hivyo kushindwa kutoa motisha kwa Bodi zenye ufanisi na hivyo kuathiri utendaji.
Sheria inayopendekezwa inapaswa kujumuisha majukumu yaliyorithiwa kutoka Consolidated Holding Corporation (CHC), ambayo yalihamishiwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kupitia Tangazo la Serikali Na. 203 la Mwaka 2014, hata hivyo hadi sasa majukumu hayo hayajajumuishwa kwenye Sheria.
Sheria inayopendekezwa inapaswa kuipa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, mamlaka ya kutoa miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa Taasisi, kwani kwa sasa Ofisi ya Msajili wa Hazina haina mamlaka ya kutoa miongozo ya kusimamia utendaji na uendeshaji wa Taasisi, badala yake Msajili wa Hazina ana uwezo wa kutoa miongozo ya kiutumishi tu kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma.