Mambo tisa yatakayoamua uchaguzi mkuu Uingereza

London. Raia wa Uingereza wakipiga kura leo kuchagua wabunge, uchaguzi huo unatazamwa kwa sera za vyama vya siasa na jinsi zitakavyoathiri mataifa mengine, hasa ya Afrika, zikiwemo sera za uhamiaji, elimu na mpango wa Rwanda kuwapokea wahamiaji.

Masuala mengine yanayopangaliwa katika uchaguzi huo ni pamoja na ukuaji wa uchumi, afya, uhalifu, ulinzi na usalama, makazi na Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya (Brexit).

Uchaguzi huo unakuja baada ya miaka mitano tangu Desemba 2019, ambapo nchi nzima ina nafasi ya kuamua chama gani kitapata viti vingine kimtoe waziri mkuu na kuunda serikali.

Vyama vinavyopewa nafasi kubwa ya kushinda ni Conservative cha Waziri Mkuu Rishi Sunak na Labor kinachoongozwa na Keir Starmer.

Vyama vingine ni pamoja na Reform UK, Liberal Democrats, Democratic Unionist Party, Green, Scottish National Party (SNP) na Plaid Cymru na vinginevyo.  

Vyama hivyo vimepiga kampeni kwa wiki sita vikinadi sera na leo mamilioni ya Waingereza wamefika katika vituo 40,000 vya kupigia kura kote England, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limeshuhudia baadhi ya viongozi wa vyama wakipiga kura, akiwemao Sunak aliyepiga kura yake North Yorkshire.

Sunak na mkewe, Akshata Murty walifika kwenye kituo cha kupigia kura ikiwa ni nusu saa baada ya vituo kufunguliwa saa 1:00 asubuhi.

Kiongozi wa Labour Sir Keir Starmer amewasili Willingham Tenants Hall, kaskazini mwa London kupiga kura yake akiwa na mke wake, Victoria.

Vituo vya kupigia kura vitabaki wazi hadi saa 4 usiku na kuhesabu kura kutaanza mara moja.

Matokeo yanatarajiwa kuanza kutangazwa saa moja baada ya kura kuanza kuhesabiwa.
 

Ikiwa chama kinashinda majimbo 326 – ambayo ni zaidi ya nusu ya idadi ya viti katika Bunge la makabwela – kitakuwa kimepata wingi wa viti unaohitajika kuunda serikali.

Kwa mujibu wa matokeo ya kura za maoni yaliyotangazwa na BBC Julai 3, 2024, chama cha Labour kilionekana kuongoza kwa asilimia 39, kikifuatiwa na Conservative (asilimia 21), kisha Reform Uk (asilimia 17), Liberal Democratic (asilimia 11), Green (asilimia 7), ANP (asilimia 3), na Plaid Cymru asilimia 1. 

Miuongoni mwa mambo yaliyozua mjadala wakati wa kampeni na huenda yakaamua ushindi ni pamoja na uhamiaji, elimu na mpango wa Rwanda.

Katika suala la uhamiaji, Conservatives na Labour Party, vimeahidi kupunguza idadi ya watu wanaohamia Uingereza ikiwa vitashinda na pia kuzuia kuingia kinyume cha sheria nchini humo.

Chama cha Conservatives kinasema uhamiaji ni mkubwa sana na kinataka kuvutia tu wahamiaji wenye ujuzi kuingia Uingereza ili kuchangia biashara zao na huduma za umma.

Kwa hivyo, wanahitaji kupunguza idadi ya watu wanaohamia nchini humo hadi viwango vinavyoweza kudumishwa ili kupunguza athari kwenye huduma za umma na makazi na pia kurejesha imani ya umma kwa mfumo huo.

Njia yao ya kufanikisha hili ni kuweka kikomo cha kisheria kwenye uhamiaji. Kinasema kitapeleka bungeni idadi ya viza za kazi na familia na idadi hiyo itapungua kila mwaka.

Wakati huohuo, Labour Party inasema itarekebisha mfumo wa uhamiaji unaotegemea pointi na kumaliza kutegemea wafanyakazi wa nje kwa muda mrefu.

Mnamo 2023, kati ya watu 1.2 milioni waliohamia Uingereza, 141,000 walitoka Nigeria. Idadi hiyo inapita ile ya nchi nyingine yoyote ya Afrika na nchi ya pili isiyo ya Umoja wa Ulaya baada ya India.

Katika elimu, hivi sasa ukiwa unasoma Uingereza, watakupa visa ya kuhitimu ambayo inakuruhusu kukaa nchini kwa angalau miaka miwili baada ya kuhitimu.

Kwa wale tu walioko kwenye programu za utafiti wa baada ya kuhitimu wanaweza kupeleka familia zao Uingereza.

Vyama viwili vikuu havikusema kwamba vitabadilisha sera hiyo, lakini kiongozi wa Reform UK, Nigel Farage anasema atapiga marufuku wanafunzi kuingiza wenza wao na watoto Uingereza.

Wakati Green Party kinasema kitairuhusu sera hiyo na pia kutoa haki ya kupiga kura kwa watu wenye viza.

Serikali ya sasa ya Conservative inataka kupeleka baadhi ya watafuta hifadhi nchini Rwanda. Hivi sasa, mkataba walionao na Rwanda ni kuhamisha wahamiaji 300 wanaovuka kwa njia haramu kwenda Rwanda.

Kwa Juni pekee, karibu watu 600 walifika Uingereza kwa boti ndogo. Kwenye ilani ya Conservative, kuna mpango wa kuanza kupeleka watafuta hifadhi hao Rwanda kuanzia Julai.

Hata hivyo, Labour inasema itaufuta mpango wa Rwanda na badala yake itaajiri maofisa wapya wa polisi wa mpakani. Pia itapambana na magenge yanayosafirisha watu kinyume cha sheria.

Wakati Liberal Democrats inasema inapendelea kutoa njia salama na za kisheria kwa watafuta hifadhi, Chama cha Plaid Cymru kinapinga mpango wa kupeleka watafuta hifadhi Rwanda.

Suala la uhamiaji limekuwa mjadala mgumu kwa siasa za Uingereza na kila chama kinajadili jinsi ya kukabiliana nalo.

Akizungumza na BBC, Dk Anthony Francis Mveyange kutoka Kituo cha Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya cha Afrika, anasema ikiwa Serikali ya Uingereza inaweza kutegemea wanafunzi, inaweza kuwatumia kwa madhumuni mengi.

Kwanza kwa ajili ya masilahi ya Afrika, wakati huohuo, kwa ajili ya masilahi ya Uingereza.

Related Posts