Aliyeshtakiwa kwa kumuua, kumzika mumewe aachiwa huru

Arusha. Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Sumbawanga, imemwachia huru Limi Shija, mkazi wa Kijiji cha Kabage, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kumuua na kumzika mumewe, Masunga Kashinje, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.

Ilidaiwa kuwa mauaji hayo yalitokana na ugomvi baina ya wanandoa hao kuhusu mashamba na ng’ombe kadhaa ambao familia ilinunua kutokana na mahari ya binti yao kuolewa.

Ilidaiwa kuwa marehemu ndiye alipanga kumuua mkewe na aliwalipa vijana wawili Sh2 milioni, lakini wa walikutana na mshtakiwa na kumweleza nia hiyo ya mumewe, hivyo naye aliwaongezea Sh2 milioni, wakaenda kumuua mume na kumzika, kisha mke akatoroka.

Hukumu hiyo imetolewa Julai 2, 2024 katika Mahakama Kuu Sumbawanga na Jaji Deo Nangela aliyesikiliza shauri hilo la mauaji namba 69/2022.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji alisema Mahakama inamuachia huru mshtakiwa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.

Kupitia maelezo ya onyo, ilielezwa kuwa siku ambayo haijulikani tukio lilipopangwa, mwanamke huyo alikuwa ameenda mnadani ambako alimuona mumewe akiwa na wanaume wawili na alipata mashaka kuwa kuna kitu kibaya dhidi yake kinaenda kutokea.

Akiwa njiani, wanaume wawili aliokuwa amewaona na mumewe, walimkamata na kumpa siri kuwa alitakiwa kuuawa saa 9 alasiri na mumewe amewalipa Sh2 milioni.

Ilidaiwa kuwa baada ya kupata taarifa hizo mshtakiwa huyo aliwashawishi wanaume hao kuwa atawaongezea Sh2 milioni ili wakamuue aliyewatuma.

Ndipo walikubaliana na mpango huo na siku hiyo waliyopanga kumuua mwanamke huyo, walienda nyumbani kwa marehemu na kumkuta nje anakula, wakamkamata kumchukua hadi mita chache kutoka nyumbani ambako walimuua na kumzika. Baada ya tukio mke huyo na watoto walihama nyumbani hapo.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Juni 18, 2024 ambapo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano na vielelezo vitatu.

Shahidi wa kwanza wa mashtaka, aliieleza Mahakama kuwa mwenyekiti wa Kijiji cha Kabage, alieleza kupotea kwa mwanamume huyo mke wake kutoweka kijijini hadi alipokamatwa Novemba mosi, 2021.

Shahidi wa pili wa mashtaka ambaye alikuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Tanganyika kwa wakati huo, SP Meshaki Philipo alieleza kuwa alipata taarifa kwa shahidi wa kwanza kuwa mshtakiwa alikamatwa katika Kijiji cha Msila.

Alidai kwamba alikwenda kumkamata mshtakiwa huyo na katika mahojiano yake ya awali, alipoulizwa alipo mumewe, alidai aliuawa na kuzikwa nyumbani kwao.

Alisema mshtakiwa huyo alieleza kuwa chanzo cha mauaji ni mgogoro wa mashamba na mahari ambayo ilikuwa imelipwa kwa familia.

Alisema Novemba 4, 2021, mshtakiwa aliwaongoza hadi alilozikwa mumewe na walipofikua mifupa ya binadamu iligunduliwa pamoja na fuvu la kichwa.

Shahidi wa tatu ambaye ni daktari alidai mahakamani kuwa alithibitisha mabaki hayo yalikuwa ya binadamu na sampuli zake zilichukuliwa kwa ajili ya kipimo cha DNA.

Shahidi wa pili alidai mshtakiwa alimwambia kwamba mumewe aliuawa na watu wawili aliowakodi na hakujua majina ya wauaji, japo aliweza kuwatambua kwa sura.

Shahidi wa tatu, alithibitishia mahakama kuwa mabaki yaliyokutwa kwenye eneo ambalo mshtakiwa aliwaonyesha, ni mabaki ya binadamu mtu mzima wa kiume.

Alisema fuvu la kichwa cha marehemu lilikuwa na ufa ulioanzia upande wa mbele kwenda chini kushoto na kwa maoni yake, kifaa butu na kizito kilitumika kumpiga kichwani na sababu za kifo ni majeraha makubwa ya ubongo na kutokwa damu.

Shahidi wa nne ambaye ni ofisa wa polisi, alidai katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa, alikiri kuwalipa wanaume hao waliokuwa wametumwa kumuua yeye na kuwa aliwaongezea Sh2 milioni, ili watekeleze azma hiyo.

Hata hivyo, sampuli zilizochukuliwa kwa ajili ya kupima DNA kulinganisha na mtoto wa marehemu hazikutosha kutoa matokeo.

Akijitetea chini ya kiapo, Limi alikanusha kuhusika na mauaji ya mume wake na kuwa anachojua yeye ni kwamba alimweleza anaenda Songea.

Alidai kuwa alikuwa akiishi vizuri na mumewe na kuwa alisikia kuhusu mashahidi wa upande wa mashtaka wakisema kwamba alimuua mumewe, jambo ambalo hakulifanya.

Alidai alipochukuliwa kutoka Kijiji cha Mpimbwe alipokuwa na wanawe, alikuta watu wengi wenye hasira wakimsubiri nyumbani huku akiwa hajui lolote, baadaye alipelekwa polisi na kufikishwa mahakamani.

Alidai hakuwa anafahamu kifo cha mumewe na kwamba anachofahamu ni kwamba alienda kutafuta mashamba mapya na kuiomba mahakama imwachie huru.

Alipoulizwa kwa nini alihama Kijiji cha Kabage, aliiambia Mahakama kwamba aliamua kuondoka na kubadilisha mahali alipokuwa akiishi na hivyo, aliacha mali zake ambazo alikuwa anapanga kuzifata baadaye.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji huyo alianza kwa kueleza kuwa kanuni za kisheria zilizowekwa kuhusu kuthibitisha kosa, upande wa mashtaka una wajibu wa kuthibitisha kesi pasipo kuacha shaka.

Alieleza kuwa ni jambo la msingi pia kwamba mtuhumiwa hawezi kutiwa hatiani kwa kuzingatia udhaifu wa utetezi wake au kutoweza kujitetea.

Jaji ameeleza kuwa kwa kuzingatia kanuni zilizotajwa, jambo ambalo mahakama inatakiwa kuzingatia ni iwapo mashtaka yamethibitishwa pasipo shaka yoyote na ushahidi unaotegemewa ni wa kimazingira.

Alisema katika mwenendo mzima, hakuna mtu aliyedai kumwona mshtakiwa akiua au hata akikodi watu kumuua mumewe.

Kuhusu sampuli zinazodaiwa kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, amesema kwa kukosekama ushahidi wa barua iliyowasilisha sampuni hizo, inakuwa ngumu kuamini kuwa sampuli yoyote ilipelekwa huko.

Kuhusu maelezo ya onyo ya mshtakiwa, Jaji alieleza kuwa maelezo hayo yanampa mashaka na kushindwa kuyatilia maanani kwa sababu yalirekodiwa kwa mfumo wa maswali ya jibu.

Huku akinukuu kesi ya Seko Samwel dhidi ya Jamhuri ya mwaka 2005, Mahakama ya Rufani iliona kuwa taarifa iliyoandikwa kwa njia ya swali na jibu badala ya kumwacha mshtakiwa aeleze au kusimulia hadithi yake, haikuwa na sifa ya kuwa maelezo ya onyo.

Jaji alieleza kuwa kutozingatia masharti ya kifungu cha 58 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, hatazingatia maelezo hayo na kuwa kukosekana kwa uzito wowote wa maana wa ushahidi kwenye kielelezo hicho na ushahidi uliosalia ni wa kimazingira.

Baada ya kupitia hoja zote, Jaji amehitimisha kuwa mshitakiwa hajapatikana na hatia, hivyo kuamuru aachiwe huru.

Related Posts