TANZANIA ni moja ya nchi za Kiafrika zinazosifika kwa kununua magari yaliyotumika hasa yale ya Kijapani na zaidi ya kampuni ya Toyota.
Unaweza kutembea siku nzima usipate gari la Kijapani lililonunuliwa likiwa jipya. Pamoja na kwamba magari hayo yametumika, kwa mtu wa kawaida kama mimi atapata mtihani kuyatofautisha na yale yaliyonunuliwa yakiwa ‘zero kilometer’ kwani mwonekano wa yote hayo hauna tofauti na pia matumizi hayana tofauti.
Magari yaliyotumika au used (tamka yuzdi) yamewasaidia sana Watanzania kwani bei zake ni nafuu kiasi cha kumwezesha mwananchi wa kawaida au mstaafu kutimiza ndoto yake ya siku moja kumiliki gari.
Magari yaliyotumika yatakupa kila unachokitaka kwenye gari lakini usipokuwa makini unaweza kuja kufilisika kwa gharama za matengenezo pindi gari litakapoanza kuchoka na kuwa tripu shamba, tripu gereji.
Pia kuna uwezekano wa wewe kuwa mmiliki wa mwisho na kama hautakuwa mmiliki wa mwisho utaliuza kwa bei ambayo haifiki hata nusu ya gharama zako za kulinunua na kulitunza. Na ukiwa mtu wa hisani, unaweza kuligawa kwa ndugu na jamaa ili likafie mbali.
Kama ilivyo ndoto ya kila mtu kumiliki gari zuri, ndivyo ilivyo ndoto ya klabu zetu vya soka kumiliki wachezaji nyota waliong’aa hapa nchini na kwingineko Afrika na duniani.
Klabu zetu, hasa zile zilizo na kiasi fulani cha fedha, zingependa kumiliki wachezaji kama walioko Al Ahly, Zamalek, Esperance, Mamelodi na kwingineko. Klabu zetu haziwezi kwenda Burundi kumnunua kijana Saido Ntibazonkiza. Hapana, watasubiri azunguke dunia kisha wamnunue akiwa anaelekea kilele cha umri wa kucheza au niseme anaanza kuporomoka kiwango.
Klabu zetu zimekuwa na woga wa kulea vipaji kwa ajili ya matumizi au hata mauzo ya kesho. Uwekezaji katika kesho unakuwa mdogo hivyo kwa kiasi kikubwa kesho ya klabu hizi inategemea vipaji vilivyolelewa mahali na kutumika kiasi cha kupatikana kwa bei ndogo au mawakala binafsi.
Hakuna klabu isiyonunua wachezaji kutoka kwingine, hasha. Hata hivyo, haina afya ikiwa klabu itafanya kazi ya kununua, kutumia na kuachia. Klabu ya mpira wa miguu inatakiwa kuwa biashara inayonunua na kuuza.
Rais wa Awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema; “Biashara ni kuuziana na kununuliana… haiwezi kuwa kununuliana tu.”
Maneno haya yana maana hata leo. Kuna klabu za Ligi Kuu ambazo rekodi zake zinaonyesha zaidi kununua wachezaji wakati uuzaji haupo au ni mdogo sana.
Tatizo la klabu kutouza wachezaji au kutopata fedha kutokana na mauzo inatokana na ukweli kwamba klabu hazijiimarishi upande wa timu za vijana. Klabu zinaandikisha vijana ili kuiridhisha TFF na utaratibu wa leseni za Klabu.
Klabu inayonunua mchezaji kwa Sh200 milioni za Tanzania inaona taabu kutenga hata bajeti ya Sh100 milioni kwa ajili ya timu za vijana. Timu za vijana zinazopuuzwa ndizo zingekuwa shamba kwa klabu kuvuna wachezaji watakaoisaidia huko mbele.
Mikataba wanayopewa wachezaji wengi wanaokuja nchini na hata wale wa ndani zinakupa picha ya kwamba kuna woga wa kupata hasara. Woga wa kupata hasara unaweza kuwa adui nambari moja wa biashara.
Mkataba wa mwaka mmoja hadi miwili kwa mchezaji ni mkataba wa muda mfupi sana hasa kwa wachezaji ambao bado ni vijana. Matokeo ya mikataba mifupi ni wachezaji kuondoka wakiwa huru kila wanapomaliza mkataba. Ni klabu chache sana hapa nchini, kama zipo, zinazoweza kujadiliana na mchezaji kuongeza mkataba wakati akiwa bado ana mkataba wa miaka miwili. Unampata mchezaji baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu, tena mchezaji bora kwenye ligi anayotoka na umri wake ni mdogo, kwa nini apewe mkataba wa miaka miwili? Huo ni woga ambao kibiashara hauwezi kulipa.
Hasara za mikataba ya muda mfupi kwa klabu ni nyingi kuliko faida. Klabu itajikuta karibu kila mwaka inatakiwa kuongeza mikataba karibu ya nusu ya kikosi chake chote. Wachezaji wazuri na ambao tayari wameonekana na wanavutia klabu nyingine wanaweza kuuma meno wasiongeze kandarasi ili mwisho wa mkataba waweze kujiuza kama mawakala huru huku wakikwepa vizingiti vya klabu. Mchezaji aliye huru anaweza kuuzika kirahisi kwa sababu biashara yake inahusisha pande mbili, yaani klabu mnunuzi na mchezaji tu.
Klabu inaweza kujikuta inakuwa ubao wa matangazo kwa wachezaji wanaotafuta njia ya kutokea.
Klabu ya Madrid ya Hispania ni mfano wa klabu iliyokuwa na falsafa ya kununua wachezaji nguli duniani au ‘galacticos’.
Ununuzi wa Alfred Di Stefano katika miaka ya 1950 ulikuwa mwanzo na kufuatiwa na ujio wa kina Zidane, Figo, Beckham, Ronaldo na wengineo. Real Madrid iliwatumia wachezaji hawa kibiashara zaidi kiasi kwamba walioonyesha upungufu uwanjani, tayari mauzo ya majina yao kwenye soko yalishaingiza pesa ya kutosha.
Falsafa ya Galacticos ilikuwa ni kuingiza Galactico mmoja au wawili kwa msimu na si zaidi. Galactico hawakupewa mkataba wa mwaka mmoja au miwili. Hata hapa Afrika, klabu kama Ahly haitoi mkataba wa mwaka mmoja kwa mchezaji iliyeangaika kumpata, yawezekana ndio siri ya kufanya vizuri katika mashindano ya CAF. Kikosi kipya kila msimu ni vigumu kujenga timu ya mafanikio, pia kifedha timu itakuwa inatumia pesa nyingi kusajili bila yenyewe kuwa na uwezekano wa kupata pesa nyingi kutoka kwenye mauzo ya wachezaji.
Ligi Kuu Bara imesifiwa kama moja ya ligi zinazofanya vizuri, hata hivyo kuna utamaduni au upungufu unaohitaji kufanyiwa kazi hasa upande wa masoko na fedha ili kuzifanya klabu ambazo ni mhimili wa ligi hiyo ziwe na uchumi endelevu.
Weledi katika fedha, masoko na utawala unatakiwa kujengeka kuanzia ligi za chini na hata akademi. Pamoja na uwepo wa fedha za wadhamini, bado mauzo ya wachezaji ni chanzo muhimu cha mapato.
Tujiulize hawa wa Ivory Coast, Senegal, Burundi na Uganda wanaotuuzia wachezaji kila siku huwapata wachezaji vijana wapi? Wachezaji huru, wachezaji wazee na wachezaji wa mkataba wa muda mfupi si rahisi kama tunavyofikiri.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.