KATIBU MKUU WAZAZI HAPI AMETEMBELEA TRENI YA MWENDOKASI DODOMA

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg.Ally Salum Hapi (MNEC) ametembelea na kuona treni mpya ya kisasa ya mwendokasi iliyowasili, Jijini Dodoma jana usiku ikitokea Jijini Dar Es Salaam iliyokuja na viongozi mbalimbali wa dini na serikali, wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Ndg.Masanja Kadogosa, pamoja na waandishi kwa ajili ya kuahiriki Dua Maalumu ya Kuliombea Taifa iliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, leo, ambapo Mgeni Rasmi Alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Phillip Isdor Mpango.

Akizungumza baada ya kutembelea na kuona ubora, uzuri na utendaji kazi wa treni hiyo, Katibu Mkuu Wazazi, Ndg.Hapi, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kutekeleza Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 – 2024 kwa vitendo na kusema anastahili kuongezewa hali, morali na moyo wa kuendelea kuwatumikia wananchi wa Tanzania.

“Kwa niaba ya viongozi, wanachama na wapenzi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM nichukue fursa hii adhimu kumpongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha mradi wa ujenzi wa reli ya mwendokasi kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma imekamilika kwa asilimia kubwa pamoja na majaribio ya treni ya mwendokasi na mabehewa yake kuletwa nchini na kuanza kufanyia majaribio yanayotoa matokeo chanya;

“Ama kwa hakika hii ni furaha na faraja kubwa sana kwetu sisi wamiliki wa duka kuona muuza duka wetu anaiendesha vizuri biashara yetu na matokeo chanya yanaonekana, lakini pia nitoe pongezi kwa watumishi wote wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa usimamizi bora wa fedha za mradi huu ambao ni Tshs.Bilioni 23.5 ni fedha nyingi mnoo ila ndugu zetu hawa wanastahili pongezi kwa kusimamia vyema fedha hizo” alisema Hapi.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa TRC, Ndg.Masanja Kadogosa, alitoa shukurani kwa viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Wazazi kwa kutembelea mradi huo kwa kusema kwao watumishi wa Shirika la Reli Tanzania hujisikia ufahari wa hali ya juu inapotokea nafasi ya viongozi wa CCM na Jumuiya zake wanapotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya mwendokasi na kusifia kwa kile kilichofanyika inawatia moyo na morali wa kuendelea kutumikia shirika na serikali kwa maslahi mapana ya nchi.

Katika msafara wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, Ndg.Hapi, aliongozana na Naibu Katibu Mkuu Wazazi Bara, Ndg.Joshua Mirumbe Chacha, viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dodoma, Wilaya pamoja na kata husika kwa kujitoa kuungana nao kutembelea na kutazama mradi huo.

Related Posts