NMB yazipiga tafu sekondari Dar kwa vifaa vya milioni 10

Benki ya NMB imekabidhi meza 90 na viti 90 vyenye thamani ya zaidi ya Sh 10 milioni kwa shule za sekondari Uhamiaji na Mchikichini za jijini Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa azma ya benki hiyo kuboresha sekta ya elimu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Samani hizo ambazo zinalenga kupunguza tatizo la upungufu wa madawati kwa walimu na wanafunzi, ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa uwekezaji wa benki hiyo kwa jamii (CSI).

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi meza na viti hivyo Jijini Dar es Salaam jana Jumatano, Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona alisema uboreshaji wa sekta ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele muhimu kwa benki  hiyo.

Pia alisisitiza dhamira ya benki hiyo ni kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wote ikiwemo Serikali katika kuinua maendeleo ya sekta ya elimu nchini kote.

“NMB tunatambua kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha ndiyo maana kwa miaka mingi tumewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuinua ukuaji wa sekta ya elimu. Kwa hakika, sekta ya elimu ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika mkakati wetu wa CSI. Huwa tunatenga asilimia moja ya Faida Baada ya Kodi (PAT) kila mwaka ili kuchangia mipango mbalimbali ya maendeleo,” alisema.

Mpona aliongeza, “Tunaamini samani tunazotoa leo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu,”

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, aliipongeza benki hiyo kwa moyo wake wa ukarimu na kusisitiza dhamira ya Serikali ni kuendeleza maendeleo ya sekta ya elimu.

“Tunafahamu kuwa shule nyingi za wilaya ya Temeke bado zinakabiliwa na changamoto nyingi na zinahitaji msaada zaidi kutoka kwa wadau wa elimu kwa kuwa tuna bajeti ndogo.

“Naishukuru NMB kwa kuunga mkono jambo hili zuri na nachukua fursa hii kutoa wito kwa wadau wengine wa ushirika kuungana na azma yetu ya kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alipokea meza 50 na viti 50 vilivyotolewa na NMB kwa Shule ya Sekondari Mchikichini, alishukuru benki hiyo kwa kuendelea kuunga juhudi za serikali za kuboresha sekta ya elimu.

“Tunasikia faraja kwa benki yetu kwa kuendelea kuwa karibu na wananchi. Rais Samia ameshaleta fedha za kujenga ghorofa katika shule hii ya Mchikichini na matundu ya vyoo. Kitendo cha benki ya NMB kutoa meza na viti ni jitihada njema za kuunga mkono serikali na siku zote wamekuwa wakituunga mkono kwa vitendo,” alisema.

Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Uhamiaji, Christopher Mtabutu alibainisha kuwa shule yake ilikuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati ya walimu hivyo msaada huo wa NMB umekuja wakati muafaka.

“Ninaamini kuwa madawati na meza ambazo benki ya NMB imetupatia leo vitasaidia kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu mbali na kuboresha usalama wa mali zao pia,” aliongeza.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mchikichini, Nelson Nestory alisema, “Tunaishukuri benki ya NMB kwa kutupatia meza 50 na viti 50 kwani sasa tumemaliza tatizo la wanafunzi kukosa meza na viti”.

Aliahidi shule hiyo kuendelea kutunza msaada huo vyema ili kusaidia vizazi vijavyo.

Related Posts