Theresa, Gaguti waula soka la wanawake Mwanza

WIKI chache baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama cha Soka la Wanawake (TWFA) Mkoa wa Mwanza, Sophia Tigalyoma amefanya uteuzi wa nafasi tano kikatiba na kukamilisha safu yake ya uongozi atakayofanya nayo kazi kusimamia soka hilo mkoani hapa.

Tigalyoma alichaguliwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Juni 8, mwaka huu jijini hapa, akishinda pamoja na Revina Muzawena (mjumbe wa mkutano mkuu taifa), Hawa Bajanguo na Flora Gaguti (wajumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho).

Baada ya siku takribani 25, juzi Tigalyoma alitangaza kuwateua Theresa Chacha kuwa katibu mkuu wa chama hicho, huku Flora Gaguti akiwa makamu mwenyekiti. Wengine ni wajumbe wawili wa kuteuliwa wa kamati ya utendaji, Hilda Mapunda na Beatrice Kapungu na Clara Kisaka akiwa mweka hazina.

Akizungumzia uteuzi alioufanya kikatiba, Tigalyoma alisema safu yake ya uongozi imekamilika na ndiyo timu ya kupambana kuendeleza mpira wa wanawake Mwanza, huku akisisitiza watu hao ni muhimu na wachapakazi, hivyo, hajawateua tu ilimradi.

“Nimeshakaa na kujaza nafasi kwa mujibu wa katiba nimeshapanga safu ili tayari tuanze kufanya kazi kikamilifu kusaidia soka la wanawake Mwanza. Mikakati yetu ni kuzungumza na kushirikiana na klabu tujue mahitaji yao na jinsi ya kupiga hatua,” alisema Sophia na kuongeza;

“Pia tutazungukia wilaya zote ziwajue viongozi wao wa ngazi ya mkoa tufanye kazi kwa kauli moja ya maendeleo ya soka.”

Related Posts