Mbeya. Kijana Shadrack Chaula (24) mkazi wa Kijiji cha Ntokela, Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya amehukumiwa faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka miwili jela akishindwa kuilipa faini hiyo kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo mtandaoni.
Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi Julai 4, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, Shamla Shehagiro.
Awali, mawakili wa Serikali, Veronica Mtafya na Rosemary Mginyi waliieleza Mahakama kuwa Juni 22, 2024 katika eneo la Ntokela mshtakiwa alisambaza video zenye taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa Tik Tok, kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandaoni.
Chaula ambaye pia ni msanii wa uchoraji, video yake ilisambaa mtandaoni Juni 22 akiwa anachoma moto picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, suala ambalo lilikemewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na kuagiza akamatwe.
Fuatilia zaidi katika mitandao ya Mwananchi