KIKOSI cha Kagera Sugar kitaanza maandalizi ya kujifua na msimu mpya Jumatatu Julai 8, mwaka huu mjini Bukoba huku kikitarajiwa kushusha mashine mpya 12 na kuweka kambi yake mkoani Shinyanga kusaka utulivu.
Mastaa wa timu hiyo walipaswa kuwasili mjini Bukoba kuanzia juzi (Jumatano) na kambi kuanza Alhamisi lakini kutokana na changamoto mbalimbali maandalizi hayo yamesogezwa mbele hadi Jumatatu ambapo timu hiyo itaanza maandalizi ya wiki moja Bukoba kisha kusafiri hadi Shinyanga.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kutua juzi mjini Bukoba kuanza maandalizi, kocha msaidizi wa timu hiyo, Marwa Chambeli alisema kwamba tayari majina ya wachezaji wapya waliowapendekeza yako mikononi mwa mtendaji mkuu na menejimenti.
Alisema katika mapendekezo hayo wanataka wachezaji wapya 12 wakiwemo wazawa 10 na wageni wawili ili kuboresha kikosi chao na kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita.
“Nimefika Bukoba jana (juzi Jumatano) tulitakiwa tuanze maandalizi kesho (jana Alhamisi) lakini tumesogeza hadi Julai 8 siku hiyo ndipo wachezaji wanatakiwa waripoti kambini,” alisema Chambeli na kuongeza;
“Tutaanza maandalizi yetu hapa Bukoba kwa wiki moja baadaye tutaangalia tutaweka wapi kambi lakini mipango iliyopo ni kusafiri kuweka kambi yetu mkoani Shinyanga.
“Kuna usajili majina yameshapendekezwa viongozi na CEO (mtendaji mkuu) wanayashughulikia, kwenye mapendekezo yetu benchi la ufundi baada ya tathmini tunataka wachezaji wapya 12 lakini wageni wasizidi watatu,” alisema.