Ishu ya Beno tatizo ni msimamo

ALIYEKUWA kipa wa Singida BS, Beno Kakolanya amemaliza utata, akisema misimamo yake imekuwa ikimponza kwa watu wakimchukulia kama mtovu wa nidhamu.

Beno aliyeondoka Singida kiutata dakika za lala salama za Ligi Kuu Bara, kwa kilichoelezwa ni utovu wa nidhamu wakati chama hilo likiwa na mechi ngumu dhidi ya Yanga, aliliambia Mwanaspoti kuwa, yeye ni mchezaji anayejitambua hivyo siku zote amekuwa akisimamia kile anachoona ni sahihi.

Kipa huyo wa zamani wa Tanzania Prisons, Yanga na Simba, alitolea mfano ishu na Yanga kwa kusema mgomo ulitokana na kutotimizwa kwa kimaslahi binafsi.

”Hapo unaweza kusemwa we ni mtovu wa nidhamu? Jibu hapana na wala sikuwahi kuwa na tatizo na kiongozi yeyote wa Yanga kwa sababu najua huu ni mpira,” alisema Beno na kuongeza;

“Kwani watu waliwahi kusikia mimi ni mtovu wa nidhamu wakati nikiwa Simba? Jibu ni hapana na niliondoka vizuri tu na wala hapakuwa na tatizo, ni vile tulishindwana tu katika mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya ndio maana nilijiunga na Singida.”

Beno alisema kilichotokea Singida, hata yeye kilimshangaza kwani aliondoka akiomba ruhusu, lakini ikaonekana tofauti.

”Ningekuwa nimeondoka kinyemela kambini bila ya sababu ya msingi hapo ndio ungeweza kusema labda ni msaliti lakini niliondoka kwa ruhusa,” alisema Beno.

Katika sakata hilo, kamati ya nidhamu ya Singida FG ilieleza kumuandikia barua Beno ili ajibu tuhuma zinazomkabili za kutoroka kambini na kuihujumu timu, ila staa huyo aligoma kuhudhuria kikao hicho.

Hata hivyo, kwa sasa ukurasa wa Beno na Singida umefungwa na inaelezwa anaweza kumalizia mkataba uliosalia akiwa Namungo kwa makubaliano maalum.

Related Posts