Ligi ya Kikapu Dar vita yaanza upya

ILE vita ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) imeanza upya wakati mechi za mzunguko wa pili zikitarajiwa kupigwa kwa watetetezi Dar City kuliamsha mbele ya Ukonga Kings.

Mchezo huo wa kibabe, utapigwa kwenye Uwanja wa Don Bosco Oysterbay keshokutwa Jumapili, utafuatiwa na michezo mingine mitano itakayowapa burudani mashabiki wa mchezo wa kikapu watakaohudhuria na wale watakaoifuatilia kupitia katika runinga kwa siku hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), Haleluya Kavalambi, imeitaja michezo mingine ya wikiendi hii ni ule wa Jeshi Stars dhidi ya UDSM Queens.

Mingine ni; DB Lioness na DB Troncatti, Pazi na UDSM Outsiders, Chui na Crows, huku mchezo wa mwisho utakuwa ni kati ya Srelio na Vijana ‘City Bulls’.

Kocha wa Dar City, Mohamed Mbwana, aliliambia Mwanaspoti kuwa,  katika mchezo dhidi ya Ukonga Kings watashuka uwanjani bila dharau kwani sio timu ya kubezwa.

“Mzunguko huu wa lala salama sio wa kudharau timu, kwani kila moja inatafuta nafasi ya kucheza  Nane Bora,” alisema Mbwana,  nyota wa Chang’ombe Boyz aliyewataja baadhi ya wachezaji nyota waliobeba tumaini la Dar City kuwa ni; Jmael Marbuary, Ally Abdalah, Bramwel Mwombe, Haji Mbegu na Josephat Peter.

Kwa upande wa Ukonga Kings, kocha wa timu hiyo, aliwataja wachezaji watakaoliamsha ili kuipambania timu hiyo ni pamoja na  Stanley Mtunguja, John Luzua  na John Kikusa, huku akitamba Dar City ijipange hiyo Jumapili.

Related Posts