AKILI ZA KIJIWENI: Mamelodi wameonyesha ukubwa kwa Mokwena

HAIKUONEKANA kama maisha yangeenda kasi kwa kocha wa mpira Rhulani Mokwena baada ya mafanikio aliyoipa Mamelodi Sundowns.

Miezi michache iliyopita aliongeza mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa miaka minne zaidi kwa kile ambacho kilitafsiriwa na wengi kwamba kuna imani ya uongozi kwa kocha huyo.

Mataji matatu ambayo aliiongoza Mamelodi Sundowns kunyakua msimu uliomalizika yalionekana yangekuwa kinga zaidi kwa kocha huyo kubakia ndani ya timu hiyo kwa muda mrefu.

Katika msimu huo wa 2023/24, Mokwena aliipa Mamelodi Sundowns taji la michuano mipya ya African Football League (AFL) kwa kuifunga Al Ahly katika mechi ya fainali, kisha akaiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) na akatwaa pia taji la MTN Super 8.

Na yeye binafsi akamaliza msimu vizuri zaidi kwa kufanikiwa kutwaa tuzo ya kocha bora wa msimu wa 2023/2024 wa Afrika Kusini, tuzo ambayo haikuonekana kama aliipata kwa kubahatisha.

Hata hivyo, juzi Jumatano, Mamelodi Sundowns ilitangaza ghafla kuachana na kocha huyo baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili na hivyo kuhitimisha utumishi wa miaka minne wa kocha huyo ndani ya timu yao.

Inaripotiwa kwamba sababu ambayo imepelekea Mamelodi kuachana na Mokwena ni mgogoro baina yake na mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo, Flemming Berg baada ya kocha huyo kulazimisha kumchezesha Matias Esquivel ambaye bosi wake anaona kama hana ubora wa kuisaidia timu hiyo.

Lakini inatajwa sababu nyingine kuwa ni tathmini iliyofanywa na uongozi wa Sundowns ambayo imeonyesha kuwa kocha huyo hawezi kuipa mataji makubwa barani Afrika timu hiyo ambayo ipo chini ya umiliki wa familia ya bilionea Patrice Motsepe.

Mamelodi inaamini kwamba kwa uwekezaji ambao imeufanya, inastahili kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na lile la Caf Super Cup maana ndio makubwa zaidi hivyo wanaamini Mokwena hana uwezo wa kuyabeba.

Wametuonyesha ukubwa wao maana hapa kwetu kuchukua Ligi Kuu tu vurugu na tambo zake sio mchezo.

Related Posts