SIO kila kocha anaweza kuwa na kipaji cha kung’amua kipaji cha mchezaji na kukipa nafasi hadi baadaye muhusika akawa nyota mkubwa wa soka.
Na hii kwa hapa kwetu inasababishwa na uwapo wa kundi kubwa la makocha ambao hawana maarifa makubwa kiufundi ambayo yanaweza kuwafanya wawe na utambuzi mzuri wa vipaji vya soka.
Lakini hata wadau wa soka tofauti na makocha wengi hatutazami vigezo halisi vya kiufundi ambavyo mwanasoka ili awe bora na mwenye mchango mkubwa kwa timu hapo baadaye anapaswa kuwa navyo.
Wengi tunaamini kwamba mchezaji ili awe mzuri basi anatakiwa awe na uwezo mkubwa wa kuchezea mpira, kupiga chenga na kanzu au kufanya mambo ambayo yatafanya jukwaa linyanyuke kushangilia.
Hii inasababisha kupoteza wachezaji wengi wazuri ambao wangekuwa na msaada sio tu kwa klabu mbalimbali bali pia timu zetu za taifa kuanzia zile za vijana hadi za wakubwa.
Hivi karibuni nyota wa timu ya taifa ya wanawake anayecheza soka la kulipwa huko Saudi Arabia katika timu ya Al Nassr, Clara Luvanga katika mahojiano yake na chombo kimoja cha habari alithibitisha hilo.
Luvanga amedai kwamba hapo awali kabla ya kujiunga na Yanga Princess, kocha wa timu mojawapo aliyowahi kuichezea alimdharau na kumnyima nafasi ya kucheza akidai hana umbile na muonekano wa kiuchezaji na hivyo kuwatumia wachezaji wengine.
Hata hivyo, kocha wa Yanga Princess, Edna Lema aligundua ubora ambao upo kwa Clara Luvanga na kuamua kumpa nafasi na baada ya hapo kilichofuata ni historia ya kuvutia kwa mwanadada huyo.
Tujikite katika kusaka maarifa ya kubaini vipaji vinginevyo tutawapoteza kina Clara Luvanga wengi.