Latra yabuni mfumo kuonyesha safari ya abiria

Dar es Salaam. Ikiwa unatarajia kupokea mgeni anayesafiri kwa basi kutoka mkoa wowote nchini, hutahitaji tena kukaa muda mrefu kituoni, kwani taarifa kuhusu basi zitapatikana kwenye simu yako.

Ni baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) kubuni Mfumo wa Habari kwa Abiria (Passenger Information System au Passenger Information Display – PIS).

PIS inaruhusu mtu kupata taarifa kuhusu eneo na muda wa kufika kwa mabasi yote ya mikoani.

Mfumo huo umebuniwa kuwapa taarifa abiria na watu wanaowapokea kwenye vituo vya mabasi.

Mkuu wa Mawasiliano wa Latra, Salum Pazzy amesema hayo alipozungumza na gazeti dada na Mwananchi la The Citizen kwenye Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF).

Amesema mfumo huo unalenga kuboresha upatikanaji na uwazi wa taarifa za usafiri.

“Tunalenga kuboresha uzoefu wa safari kwa abiria kwa kuhakikisha wanapata taarifa sahihi, wanaweza kupokea wageni na kupanga safari zao kwa urahisi na kujiamini zaidi,” amesema.

Pazzy amesema, “Kwa kuanza, Latra tayari imeweka PIS kwenye Kituo cha Mabasi cha Magufuli na Kituo cha Mabasi cha Job Ndugai. Kwa sasa tunajaribu mfumo huu, lakini kadri muda unavyosonga, tutafunga skrini kwenye vituo vikuu vya mabasi kote nchini, watu wanaweza kuona kinachotokea kwa basi gani.”

Amesema mfumo huo ni programu inayotumia wavuti ambayo mtumiaji au yeyote mwenye simu janja, kompyuta au kifaa kingine chochote anaweza kutafuta kupitia tovuti ya Latra na kupata taarifa.

Ametoa mfano kuwa, mtu akiwa kwenye Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam akitarajia kumpokea mgeni, anahitaji kuchagua programu ya kituo na PIS itaonyesha mabasi, likiwamo husika analolisubiri, eneo lilipo na muda unaokadiriwa wa kufika kwa kutumia simu.

Kupitia program hiyo, amesema hakuna haja ya kumpigia simu dereva au kondakta kuuliza basi liko wapi.

“Ni sawa kabisa na ile ya kwenye viwanja vya ndege ambako tunaweza kuona ndege zinavyokuja na muda unaotarajiwa wa kufika na kuondoka pia. Hii itatumika kwa mabasi yote ya mikoani,” amesema.

Amesema Latra inahimiza umma kuanza kutumia mfumo huo na kutoa maoni kwa mamlaka kuhusu wanachotaka kiboreshwe kulingana na utendaji wake wa sasa.

“Mfumo huu ni tanzu wa Mfumo wa Kufuatilia Magari (VTS) ambao umeunganishwa na mabasi yote ya miji, na mabasi yatakuwa na nafasi ya kuingiliana na PIS,” amesema.

Amesema hadi sasa, zaidi ya mabasi 10,000 ya mikoani yamefungwa VTS, mfumo ambao amesema umesaidia katika usalama wa abiria.

Mfumo wa VTS, ulianza kutumika mwaka 2017 ambao husaidia kufuatilia mwenendo wa gari kwa kuweka kifaa ndani ya gari husika.

Kifaa hicho kina uwezo wa kupata mawasiliano kutoka kwenye satelaiti zinazokisaidia kujua sehemu gari lilipo na ndani yake kinatumia kadi ya simu yenye uwezo wa kutumia taarifa au data za mitandao ya simu kutuma taarifa.

Mkazi wa Kimara, Judith Chuwa, aliyetembelea banda la Latra kwenye maonyesho hayo amepongeza hatua hiyo akisema itasaidia ndugu wa abiria kuokoa muda wanaotumia kusubiri kwenye vituo vya mabasi.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Latra (Latra CCC), Daud Daudi ameipongeza mamlaka kwa mpango wa PIS.

“Ni kitu ambacho tumekuwa tukikisubiri hasa kwa sababu kinawapa abiria fursa ya kupata taarifa. Pia itaboresha huduma kwa watumiaji kwa sababu watapata taarifa halisi kuhusu muda unaotarajiwa wa basi kufika,” amesema.

Related Posts