Lushoto. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimehitimisha ziara ya siku sita mkoani Tanga huku mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema akiishauri Serikali kuweka sera nzuri ya wakulima wa matunda kukopeshwa kupitia hati ya ardhi ya mashamba yao.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho leo Alhamisi Julai 4, 2024 kwenye Operesheni +255 wilayani Lushoto, Lema amesema Serikali inatakiwa kuwapa hati za ardhi wananchi ambao wana mashamba, lengo ni kuwa na uwezo wa kwenda benki kukopeshwa.
Amesema Mkoa wa Tanga una fursa nyingi za kilimo lakini wakulima wake wengi hawalimi kilimo bora na wale wanaozalisha matunda hawana soko la uhakika badala yake wanauza matunda yao barabarani, kitendo kinachowakosesha faida.
Lema ameongeza kuwa katika wilaya nane za mkoa wa Tanga ambazo wamepita hakuna sehemu wamekosa kuona ardhi bora, ambayo inakataa kilimo chochote kile, lakini bado haina faida kwa wananchi wake.
“Bado sera ya kukopa benki kwa wakulima hapa nchini si rafiki, inatakiwa mkulima akopeshwe halafu alipe baada ya kuvuna, lakini sio utaratibu wa mkulima kukopeshwa ikiwa hajaanza kuvuna, anatakiwa kuanza kurejesha, sera ambayo inasababisha wakulima wanaishia kuuza matunda barabarani,” amesema Lema.
Awali, mwenyekiti kamati ya hamasa ya Chadema mkoa wa Pwani, Ali Mohamed amewaomba wananchi kukiunga mkono chama hicho kwani kina sera nzuri ya kilimo ambayo itawakomboa wakulima wa matunda.
Ametolea mfano Wilaya ya Lushoto akisema wananchi wake ni wakulima wazuri wa matunda, lakini mazao yao hayana faida kwao kwa kuwa hakuna soko la uhakika na hivyo matunda yao kuharibika haraka.
Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewashukuru wananchi waliojitokeza kwenye mikutano yake na kuwataka kukiunga mkono chama hicho kuleta mabadiliko kwenye maeneo yao.
Pia Mbowe amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kusimamia vizuri mikutano yake na kuwa kama kuna changamoto zimetokea ni za kibinadamu, lakini mikutano yote kwenye wilaya sita za Tanga zimekwenda vizuri.
Moja ya hoja kubwa ambazo zimeibuka kwenye mikutano wa Chadema wakiwa kwenye Mkoa wa Tanga, ni kutekwa kwa kada wa chama hicho Kombo Mbwana ambaye hajapatikana, na hivyo viongozi hao kumwomba Rais Samia kuingilia kati.