MWEKEZAJI wa viwanda na mashamba ya chai yaliyopo mkoani Iringa na Njombe amesema Kampuni ya DL Group ipo mbioni kulipa mishahara ya miezi miwili kwa wafanyakazi wake wote wa viwandani na mashambani ndani ya siku saba kuanzia leo tarehe 4 Julai 2024. Anaripoti Mwandishi Wetu, Njombe…(endelea).
Akizunzungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi miongoni mwa wakurugezi wa Kampuni ya DL Group inayomiliki viwanda vya kuchakata chai vya Itona, Kibena, Ikanga na Luponde, Colins Otieno amesema kuporomoka kwa soko la chai duniani na kuadimika kwa dola kumechangia ucheleweshwaji wa malipo ya mishahara kwa wafanyakazi.
“Soko la chai Afrika Mashariki limezidi kudorora kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na Urusi, Israel na Palestina ambapo mataifa hayo nimiongoni mwa wanunuzi wakubwa wa chai inayozalishwa afrika Mashariki,” amesema Otieno, na kuongeza kuwa kuadimika kwa dola kumechochea kushuka kwa soko la chai duniani.
Amesema wamekuwa wakipata dola ya Kimarekani 0.6 kwa kilo kwenye mapato ya hisa ya chai ambayo ayaendani na gharama wanayoitumia kwenye uzalishaji na hivyo imechangia kwa kiasi kikubwa kampuni kushindwa kulipa mishahara kwa wakati ambapo ameahidi muarubaini wa tatizo hilo kwani litapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“DL Group imejipanga kufanya kazi na serikali na vilevile tunatambua mchango wa Waziri wake wa Kilimo, Hussein Bashe, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka na Bodi ya Chai Tanzania,” alisema Otieno, na kuongeza kuwa kampuni yake inaendelea na mazungumzo na serikali kuona namna itakavyo wajengea uwezo wakulima wadogo wadogo na wafanyakazi wake ili kuinua sekta ya chai nchini.
Kwa mujibu wa Otieno alisema DL Group kwa kushirikiana na serikali inakusudia kuboresha maisha ya wakulima wadogo wadogo ambapo itaiuzia serikali mashamba yake matatu ili kuwapa wakulima wadogo ambao ni miongoni mwa wale watakao nufaika na mafunzo yatakayo tolewa na kampuni ya KenyaTanzania Development Authority (KTDA).
“Tupo kwenye mazungumzo na kampuni ya Kenya Tanzania Development Authority (KTDA ambayo ina viwanda 70 na wakulima zaidi ya laki saba (700,000) hivyo wakulima wadogo wadogo watajengewa uwezo wakuzalisha zaidi na kuwa na soko la uhakika,” alisema Otieno.
Pia alipongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya kilimo ambayo inamchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini.
Alisema kuyumba kwa soko la chai sio Tanzania pekee bali ni afrika mashariki na dunia kwa ujumla hivyo basi haipaswi wanasisa wachache bila kufanya utafiti na kujua tatizo lipo wapi badala yake wanakuwa chanzo cha kuleta migogolo baina ya wawekezaji na wafanyakazi.
Naye Michael Mwenda ambaye ni mafanyakazi wa kiwanda cha Kibena akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, amempongeza muwekezaji wa kiwanda kwa kuchukua hatua madhubuti na kuwahakikishia wafanyakazi kulipwa stahiki zao ndani ya kipindi cha siku kumi.
“Pamoja na matatizo mbalimbali yanay ikabili sekta ya chai, DL Group imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaboresha maslahi ya wafanyakazi. hiki kilichotokea hapa katikati ni kitu ambacho atukutarajia lakini huko mbele dalili ni njema,” alisema Mwenda.
Kampuni ya DL Group mpaka sasa hivi ishawekeza zaidi ya kiasi cha shilingi za kitanzania zaidi ya Bilioni 25 inamiliki mashamba Tisa (09) katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa na Njombe sambamba na kumiliki viwanda vya kuchakata chai cha Itona kilichopo Mufindi, kiwanda cha Kibena (Njombe) na Ikanga (Lupembe).