Dar es Salaam. Wakati watumiaji wa mtandao wa intaneti wakizidi kuongezeka nchini, wadau wa sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameshauri watoa huduma hizo watafute njia mbadala pale inapotokea hitilafu.
Msingi wa hoja hiyo umetokana na sakata la kukatika kwa mtandao wa intaneti Tanzania kwa zaidi za siku mbili kuanzia Mei 12, 2024 lililosababishwa na kukatika kwa kebo za intaneti za baharini.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Julai 4, 2024 katika mdahalo wa X space ulioandaliwa na kampuni ya Vodacom uliojikita kujadili huduma za upatikanaji wa mtandao wao.
Hoja hiyo, ilitolewa na Emmanuel Mwaki ambaye alishauri kuwapo kwa njia mbadala wa kebo hizo za majini kwani kukosekana kwa huduma huyo kunaleta hasara kubwa kwa Watanzania waliojiajiri mtandaoni.
“Katika suala la intaneti mnatakiwa mjue kuwa hii sasa hivi sio anasa tena bali ni ajira za watu, kuna watu tumejiajiri huku (mtandaoni), kwa hiyo lazima muwe na njia mbadala linapotokea tatizo,”amesema Mwaki
Akizungumzia hoja hiyo, Mkurugenzi wa Teknolojia Kampuni ya Vodacom Tanzania, Andrew Lupembe amesema wanashirikiana na wadau wengine kutafuta njia mbadala ila kwa sasa wanaongeza idadi ya kampuni za kebo za intaneti zinazowapa huduma ili ikitokea hitilafu kuwepo na nyingine za kutoa huduma.
“Kwa sasa njia mbadala tunayoiangalia ni kuwa na kebo nyingi ili ikifeli moja ubaki na nyingine lakini, na lazima ziwe na njia mbalimbali (multiple route) ili huduma iwe na uhakika na ya ubora.
“Katika tukio lililoteka Mei, Tanzania tuna mifumo ya kebo miwili yote ipo baharini ambayo pia sisi kama watoa huduma tumejiunga na hizo zote, mmoja ilikatika muda sana tangu Februuari, sisi tukawa tunatumia moja za upande wa Afrika Kusini, Mei nazo za upande huo zikakatwa na meli,”amesema Lupembe.
Lupembe amesema tayari wameshaingia makubaliano na kampuni nyingine ya kebo ili wawe nazo tatu kwa ajili ya kujihakikishia zaidi japokuwa bado amesema hazitoshi ukilinganisha na nchi jirani ya Kenya ambao wanazo sita.
“Lakini bado tunatafuta njia nyingine, pia tunashirikiana na wadau kama watu wa mkongo wa Taifa ili kuona namna ya kumaliza tatizo hili,”amesema Lupembe.
Akizungumza katika Mdahalo wa Mwananchi Space unaoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuhusu hatua za Serikali kupambana na kadhia hiyo ya kukatika intaneti isijirudie, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema:
“Serikali inaona umuhimu wa kuwa na satellite yetu na tupo hatua nzuri na suala la ununuzi wa satelite ya nchi si kama kununua nyanya ni mchakato wa muda mrefu.
“Tulianzisha hili kwenye bajeti iliyopita, tumeanzisha kamati, tupo hatua za mbele sana kufikia kuwa na satelite yetu,” alisema Nape.
Pia alisema, Serikali imesikia wachangiaji wengi wakikiri tunauelewa mdogo wa masuala ya mawasiliano na changamoto, hii inaweza kusababisha taharuki: “Hivyo nimepokea ushauri wa Serikali kuendelea kutoa elimu.”
“Serikali tunajenga chuo kikubwa Dodoma kwa kushirikiana na Wakorea na nyingine Kigoma halafu tutakuwa na vituo atamizi nane kwa ajili ya kufundishia masuala haya ya Tehama,” amesema Nape.
Mbali na suala la mtandao wa intaneti, pia Lupembe alisema kampuni hiyo inaendelea na mpango wa kuongeza idadi ya simu janja kwa wananchi ili watumiaji waongezeke.
“Kuna programu ya miliki simu lipa mdogo mdogo, yenye lengo ni kukuza idadi ya watumiaji wa mtandao ambao wanatakiwa watumie simu janja, sisi tuna lengo la kuongeza simu janja kwa wananchi, kitakwimu sisi (Tanzania bado tupo nyuma) katika umiliki wa simu janja.”