SHIRIKA la Marie Stopes kwa kushirikiana na Msanii wa bongo flavour na muanzilishi wa kipepeo mweusi , Mwansiti Almas watoa elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana 100 wanaotokea maeneo mbalimbali mkoani Dar es salaam.
Mafunzo haya yalifanyika katikati ya wiki hii na masomo mbalimbali yalifundishwa ikiwemo uzazi wa mpango, Saratani ya mlango wa kizazi na magonjwa ya zinaa.
Wasichana walipata fursa kukutana na mtaalamu wa afya kwa ajili ya ushauri.
Wakati akitoa mafunzo hayo Muwezeshaji wa maswala ya afya ya uzazi toka shirika la Marie Stopes Dr. Lerise Mashingo alisema kuwa elimu iliyotolewa itawasaidia mabinti kuepuka magonjwa ya zinaa na kujiepusha na mimba za utotoni.
Dkt Mashingo alisisitiza kuwa umri huu wa mabinti wanatakiwa kupata elimu ya kujitambua na afya ya uzazi kwa ujumla kutokana na kizazi cha sasa kuwahi kujiingiza katika masuala ya ngono.
Aidha aliongeza kuwa kumekuwa na muamko kubwa kutokana na shirika la Marie Stopes kuzunguka na kufanya makongamano mbalimbali katika maeneo yenye mikusanyiko kwa ajili ya kutoa elimu ya Afya ya uzazi.
Nae Mwasiti alisema kuwa semina hiyo itawasaidia watoto kufikia ndoto zao kutokana na kufundishwa mambo ambayo hayatakatisha ndoto zao.
“Kwasababu kiukweli kabisa mimi ni mwanamke, najua vitu ambavyo watoto wa kike wanakutana navyo sana na Marie Stopes ni shirika kubwa sana na huduma zake zinajulikana na ziko vizuri” Alisema Mwasiti.