Dodoma. Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) limesema ili Tanzania iweze kupanda zaidi daraja la uwezo wa kukopesheka (credit rating) na hivyo kuvuta uwekezaji zaidi ni lazima kuboresha usimamizi wa uchumi.
Julai 2024, Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na ufanyaji tathmini kwa nchi kujua uwezo wake wa kukopesheka (Fitch Rating) ilieleza kuwa Tanzania bado ina uwezo zaidi na kulipa madeni hayo vizuri.
Tathimini hiyo ilifuatia iliyofanyika, Machi 2024, Kampuni ya Moody Analytics inayofanya kazi kama hiyo ilitoa ripoti yake iliyoeleza mwenendo wa uchumi Tanzania inakopesheka na ina uwezo wa kulipa madeni.
Moodys baada ya kufanya mapitio ilipandisha daraja la uwezo wa kukopesha kwa Tanzania kutoka B2 ikiwa na mtazamo chanya (Positive Outlook) hadi B1 ikiwa na mtazamo thabiti (Stable outlook), daraja la mbali ni la juu kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.
Mchumi Mkuu kutoka Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP), kanda ya Afrika, Raymond Gilpin ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 4, 2024 alipokuwa akizungumzia kujenga uwezo juu ya kuangalia namna ya kuipandisha daraja la uwezo wa kukopesheka.
“Ili kupata daraja bora cha mikopo, nchi inapaswa kuboresha usimamizi wa uchumi. Hii inajumuisha ukuaji wa uchumi, kiasi cha akiba za kigeni na kupunguza mabadiliko katika kiwango cha ubadilishaji wa fedha,” amesema.
Amesema hiyo ni kwa sababu mambo hayo yanatuma ishara kwa wawekezaji kwamba hiyo ni sehemu ambapo uwekezaji unakuwa na hatari ndogo na hivyo kuja kwa wingi kuwekeza.
Gilpin amesema kwa kadri ishara hizo zinavyokwenda, wakala wa mikopo ataongeza kiwango cha mikopo ili kuvutia zaidi uwekezaji.
Ametaja jambo jingine katika kuboresha usimamizi wa uchumi wa nchi ni kuwa na Serikali pamoja na taasisi zinazowezesha uchumi kukua, kuwezesha biashara kufanyika na kuzingatia viwango vya riba vinavyotumika kwa mikopo.
Gilpin amesema mambo mengine ni muhimu kupata takwimu (database) ambayo wakala wa wa tathimini ya madaraja ya uwezo wa ukopeshaji atatumia katika kufanya uamuzi.
“Nchi nyingi zina data lakini si sahihi au si iliyounganishwa vizuri. Pia, baadhi ya nchi hukusanya data lakini si kwa wakati unaofaa, kwa hiyo kuna umuhimu katika kulifanya hili,” amesema.
Gilpin amesema ingawa Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika nyanja za kiuchumi lakini inataka kuwa na uwekezaji mwingi kwenye miundombinu, nishati na huduma za kijamia.
Amesema awali baadhi ya nchi za Afrika zinalipa riba ya zaidi ya mara 10 kutokana na daraja la ukopeshaji kuwa sio zuri na ndio maana UNDP imekuja na mafunzo hayo yakujenga uwezo ili kuwaimarisha kwenye eneo hilo.
“Zaidi watu milioni 7 wanaishi katika nchi ambazo zinalipa zaidi kuhudumia mikopo kuliko wanavyowekeza katika elimu na afya. Hiyo si sawa, wanatakiwa kubadilika. Na jinsi ya kubadilika katika hili ni kupata daraja sahihi,”amesema Gilpin.
Kwa upande wake, Mkuu wa UNDP nchini Tanzania, Shigeki Komatsubara amesema Tanzania inafanya vizuri katika eneo hilo lakini ina bado inayo fursa na uwezo wa kufanya vizuri kwa kuwashawishi wanaofanya tathimini hizo kwamba iko vizuri zaidi.
“Kama tutaweza kuwashawishi watu hao, tutashawishi wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini Tanzania. Pia itawezesha Tanzania kuvutia uwezeshaji mwingi kwa ushindani,” amesema.
Mshauri Mkuu kutoka Shirika lisilo la kiserikali la AfriCatalyst, Amani Mhinda amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa daraja la uwezo wa kukopesheka linakuwa bora ili kupunguza mzigo wa madeni kwa nchi za barani Afrika.
“Daraja zuri la uwezo wa kukopesheka linasaidia sana fedha nyingi zinazopatikana kwa njia ya mkopo kubakia kwenye maendeleo ya nchi za barani Afrika badala ya kwenda kwenye riba. Hakuna nchi ambayo inaendelea kwa fedha zao kwa hiyo hili ni jambo muhimu litakaloongeza imani kwa wawekezaji na wabia wa maendeleo,” amesema.