Kukosekana elimu sababu watu kukimbia majiko ya umeme

Dar es Salaam. Wakati kampeni ya matumizi ya nishati safi ikiendelea kupigiwa chapuo kila sehemu, Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) umesema kukosekana kwa elimu ni sababu ya watu wengi kuogopa kutumia majiko ya umeme kupikia, huku ikiwataka wananchi kuacha woga.

Wito huo unatolewa ikiwa ni kampeni ya  matumizi ya kuni na mkaa ili  kuunga mkono azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha asilimia 80 ya wanawake Tanzania wawe wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2030.

Wito huu pia unatolewa wakati ambao tayari Rea imesaini mkataba na Jeshi la Magereza kwa ajili ya kujenga miundombinu ya uwezeshaji wa matumizi ya nishati mbadala katika magereza 129.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Alhamisi, Julai 4, katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mhandisi wa Idara ya Mipango na Utafiti kutoka Rea, Evance Kabingo amesema wakati wakisambaza umeme katika maeneo ya vijijini wamekuwa wakihakikisha wanatoa elimu kwa Watanzania juu ya namna wanavyoweza kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kupika. Pia wakiwaeleza athari zitokanazo na matumizi ya kuni ikiwamo kuathiri afya zao na uharibifu wa mazingira.

Amesema kukosekana kwa elimu hiyo imekuwa changamoto kubwa kwa watumiaji wa majiko ya umeme kutokana na kutojua matumizi sahihi.

“Hofu kuu ni watu kujua namna gani wanaweza kutumia majiko hayo, wawe salama ndiyo maana kampuni tunazoshirikiana nazo katika kutoa haya majiko zimekuwa zikitoa pia elimu ili kuhakikisha watu wanaachana na matumizi ya mkaa na kuni kupikia,” amesema Evance.

Amesema watu wanatakiwa kutambua matumizi ya jiko ya umeme ni kama majiko mengine.

Evance amesema tayari mifumo ya majiko hayo inajiendesha yenyewe kwani ukibonyeza kitufe ili mashine iwake, na jiko hufanya kazi hapo hapo ila inahitaji mtumiaji anapaswa kufuata maelekezo.

“Kama unataka kupika maharage, wali kuna maelekezo ambayo unapewa ili uweze kupika hadi kuivisha ni teknolojia ambazo zimeboreshwa,” amesema Evance.

Jitihada hizo zinalenga kuondoa athari wanazokutana nazo watumiaji wa kuni ambapo inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 30,000 hadi 45,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati hatarishi.

Akizungumzia kuhusu magereza kutumia nishati mbadala, Mhandisi Mwandamizi Deusdedit Malulu amesema katika ujenzi wa miundombinu hiyo jumla ya Sh35 bilioni zinatarajiwa kutumika ambapo kati ya fedha hizo Sh26.5 bilioni zitatolewa na Rea huku Magereza wakichangia asilimia 24.6 iliyobakia.

Kwa mujibu wa Malulu mradi huo utakuwa wa miaka mitatu na tayari umeshaanza kutekelezwa katika magereza tofauti.

“Pamoja na miundombinu hiyo tutawajengea miundombinu ya Biogas kwa ajili ya kupikia, pia mitungi 5,920 ya gesi itagawiwa kwa watumishi wa magereza ili waanze kutumia nishati safi,” amesema Malulu.

Related Posts