Morogoro. Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za Manispaa ya Morogoro wamekuwa wakikumbana na adhabu za walimu kutokana na kuchelewa kufika shule, jambo waliloeleza linasababishwa na kukosa usafiri.
Wanafunzi hao wamesema baadhi ya makondakta wamekuwa wakikataa kuwapakia kwa madai wakidai nauli ya Sh200 ni ndogo.
Pamoja na kuchelewa kufika shule, wanafunzi hao wa shule za msingi na sekondari pia huchelewa kurudi nyumbani, wamekuwa wakionekana kwenye vituo vya daladala hadi nyakati za usiku.
Mmoja wa wanafunzi, Faidhat Yasin, amesema baadhi ya makondakta wanawazuia kupanda daladala na kuwapa kipaumbele watu wazima pekee.
“Wapo wanafunzi wanaochagua daladala za kupanda, lakini kundi kubwa linazuiwa kupanda hadi mtu mzima awatetee,” alisema Faidhat.
Mwanafunzi mwingine, Rajabu Yusuph, alisema daladala za Kihonda na Mkundi zimekuwa zikikataa kuwapakia wanafunzi kwa sababu ya abiria wanaolipa Sh700.
Alisema baadhi ya daladala zinapakia wanafunzi bila shida, lakini nyingi zinawabagua.
Mkuu wa Shule ya Msingi Msamvu A, Michael Daniel, alisema uchelewaji wa wanafunzi shuleni ni changamoto kubwa na wakati mwingine wazazi hupiga simu kuulizia watoto wao waliokosa kufika nyumbani.
Alieleza kuwa uchelewaji unasababisha wanafunzi kutumia visingizio vya usafiri kuchelewa kwenye maeneo yasiyo salama.
“Baadhi ya wanafunzi wanatumia visingizio vya usafiri kuchelewa kwenye maeneo yasiyo salama. Hivyo, tunatoa adhabu ili wasione kuchelewa ni jambo la kawaida,” alisema Daniel.
Daniel aliongeza kuwa vitendo vya makondakta kuwazuia wanafunzi vinaweza kusababisha matukio ya ukatili, hasa pale wanafunzi wanapobaki kwenye vituo vya daladala hadi usiku au kuomba lifti kwa madereva wa bodaboda au magari madogo.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Manispaa ya Morogoro, Mohamed Issa, alikanusha madai kwamba makondakta wanawazuia wanafunzi kupanda daladala, akisema wanafunzi wa sekondari wanachagua daladala zenye muziki na kukataa zisizo na muziki.
Ofisa Leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Deogratius Mhangilwa, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema wamekuwa wakichukua hatua za kukabiliana nayo, ingawa madereva wanakiuka sheria pindi maofisa wanapoondoka barabarani.
Mhangilwa aliwataka madereva kujiepusha na ukiukwaji wa sheria za leseni kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.