HATIMAYE Wekundu wa Msimbazi, Simba wamefikia makubaliano na Racing Club Abidjan ya Ivory Coast kwa ajili ya kupata huduma ya beki wa kati, Chamou Karaboue, 24, huku Ahoua Jean Charles akitajwa kuwa nyuma ya dili hilo.
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa Karaboue amekubali ofa ya kusaini Simba mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mmoja na muda wowote atatua nchini kwa ajili ya kuungana na Ahoua ambaye msimu uliopita aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Ivory Coast (MVP) huku akifunga mabao 12 na ametoa asisti tisa.
Viongozi wa Simba walifikia uamuzi wa kuhamia kwa beki huyo baada ya hesabu zao kukwama kwa Mkongomani, Nathan Idumba Fasika ambaye msimu uliopita aliichezea kwa mkopo Valerenga ya Norway akitokea Cape Town City ya Afrika Kusini.
Chanzo cha kuaminika kimeliambia Mwanaspoti kuwa Karaboue yupo katika hatua za mwisho za kuwa mchezaji rasmi wa Wekundu wa Msimbazi baada ya viongozi wa timu hiyo kumalizana na klabu yake Racing Club Abidjan.
“Simba imewafanya machaguzi mazuri ya wachezaji kwa Ivory Coast kwa sababu Charles ni MVP na Karaboue ni kati ya mabeki bora, nadhani wanaweza kuwa msaada wakati ambao wanajenga upya kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao, nikuhakikishie tu kuwa beki huyo yupo njiani (jana) kuja Tanzania,” kilisema chanzo hicho.
Uamuzi wa Karaboue kukubali ofa ya Simba inaelezwa kwamba umechochewa na Charles ambaye siku chache zilizopita alitambulishwa kuwa mchezaji mpya wa Wekundu wa Msimbazi hivyo anaamini kuwa hatokuwa mpweke akiwa na timu hiyo.
Akiongelea ubora wa beki huyo, mwandishi wa michezo Ivory Coast, Martin Zokora alisema ni mtulivu na mwenye matumizi mazuri ya nguvu na akili.
“Kati ya sifa alizonazo ni mchezaji kiongozi lakini pia ana uwezo mzuri wa kutumia nguvu na akili, alikuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Racing Club Abidjan kilimaliza msimu katika nafasi ya tatu,” alisema.
Racing Club Abidjan iliyoruhusu mabao 27 ikiwa na beki huyo katika ukuta wake imeshika nafasi ya tatu kwa timu zilizoruhusu mabao machache zaidi msimu uliopita ya kwanza ni ASEC Mimosas (15), kisha Stade d’Abidjan (24).
Karaboue ataungana na Che Malone, Hussein Kazi, Lameck Lawi (usajili wake una utata bado) na Abdulrazack Mohamed Hamza ambaye naye ni usajili mpya kutoka Super Sport United ya Afrika Kusini katika safu ya mabeki wa kati wa Simba huku ikiwa imeachana na Hennock Inonga na Kennedy Juma.