AKILI ZA KIJIWENI: Mzize akaze buti haswa msimu ujao

MDOGO wangu Clement Mzize hajamaliza msimu wa 2023/2024 kinyonge, kwani amekuwa mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho la CRDB akipachika mabao matano huku akiiwezesha Yanga kutwaa ubingwa.

Hakuwa na takwimu nzuri katika Ligi Kuu kwa vile alifunga mabao matano na hii haikuwa kwake pekee bali hata kwa washambuliaji wengine wa Yanga, Kennedy Musonda na Joseph Guede.

Hata hivyo, unaweza kumtetea Mzize kwa kutofanya vizuri katika ligi kwa vile hakupata muda mwingi wa kucheza kama ambavyo alipata katika Kombe la Shirikisho Tanzania ambalo kwa misimu mitatu mfululizo amekuwa akifanya vizuri.

Ukiangalia umri wake na kile ambacho amekuwa akikifanya kwenye Kombe la Shirikisho Tanzania utakubaliana na mimi kwamba Mzize ni straika ambaye anaweza kufanya vizuri ikiwa anapata nafasi ya kutosha na mazingira yasiyo na presha kubwa.

Kombe la Shirikisho Tanzania ni jukwaa ambalo Mzize linamtangaza sana na analitumia vizuri kwa vile huwa anapewa muda mwingi wa kucheza na benchi la ufundi kulinganisha na Ligi Kuu ambayo mahitaji ya Yanga ni makubwa kuchukua taji lake jambo ambalo linafanya kijana huyo asipewe dakika nyingi.

Kwa wanaokumbuka hata msimu wa nyuma yake, Mzize alimaliza nafasi ya pili ya wafungaji akiwa na mabao sita katika Kombe la Shirikisho, akizidiwa moja na Andrew Simchimba aliyekuwa Ihefu aliyemaliza kinara akifunga saba, kuonyesha michuano hiyo ni kama yake na ndio maana haikuwa ajabu kumaliza kinara kwa msimu uliomaliza.

Sasa msimu ujao natamani kuona unakuwa wa kitofauti kwa Mzize na anapaswa kufanya kazi ya ziada ili awe mchezaji tegemeo na muhimu katika kikosi cha Yanga kwenye Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa badala ya kusubiria Kkombe la Shirikisho tu.

Najua hatokuwa na kibarua chepesi maana Yanga imezidi kuongeza vyuma pale mbele katika dirisha la usajili ambalo linaendelea kabla ya kuanza msimu mpya.

Kaongezeka pale Prince Dube lakini pia analetwa Jonathan Sowa hivyo hakutakuwa na kazi lelemama kwa Mzize.

Related Posts