Nyoni, Kagere bado wapo sana Namungo

WAKATI baadhi ya nyota walioitumikia msimu uliopita wakianza kuondoka klabuni, mabosi wa Namungo wameamua kuuma jongoo kwa meno kwa kuwazuia wachezaji wakongwe Erasto Nyoni na Meddie Kagere kwa lengo la kuwafanya kama viongozi wa wenzao ndani ya kikosi hicho.

Chanzo cha ndani kutoka Namungo, kinasema awali nyota hao wa zamani wa Simba walikuwa wafyekwe hasa Kagere aliyeifungia timu hiyo mabao mawili akiicheza kwa mkopo wa miezi sita kutoka Singida FG, lakini simu ya mmoja wa vigogo wa klabu hiyo ilibadilisha kila kitu.

“Kuna kigogo wa juu, ametoa amri, wachezaji hao kusalia kikosini, kwani anaona kwa uzoefu wao watakuwa msaada mkubwa dhidi ya wenzao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Mfano Nyoni alipojiunga akitokea Simba, amekuwa akiwajenga wachezaji  ambao ni wadogo kwake, baadhi walikuwa na mabadiliko makubwa, hivyo tumeona ni mtu ambaye siyo wa kumpoteza.”

Kuhusu Kagere chanzo hicho, kilisema anapewa barua ya kuachana na Singida Fountain Gate, hivyo wataanza naye mazungumzo mapya ya kuwa mchezaji wao.

“Awali alikuwepo hapa kama mchezaji wa mkopo, ila hivi karibuni alikuwa anafuatilia barua yake kutoka Singida,” alisema.

Ukiachana na Nyoni na Kagere, mchezaji ambaye alikuwa anaongoza kwa kufunga mabao matano ndani ya kikosi hicho, Pius Buswita pia anaweza akaongezewa mkataba mpya baada ya kuisha wa awali, huku akitajwa pia kuwindwa na Dodoma Jiji iliyo katika hatua nzuri ya kumnyakua kutoka kwa Wauaji wa Kusini hao.

Related Posts