JINA la Athuman Masumbuko ‘Makambo’ lilianza kujulikana na kutambulika kwenye michuano ya Ligi ya Vijana U-20 ambayo ipo chini ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Wakati huo, Makambo alikuwa Mtibwa Sugar ya vijana ambayo iliweka rekodi ya kipekee kwa miaka ya hivi karibuni ikibeba ubingwa mara tano mfululizo kuanzia 2018.
Msimu uliopita alifanya vizuri kwenye mashindano hayo akichukua tuzo ya mfungaji bora akiweka kambani mabao saba.
Baada ya kufanya vizuri msimu uliofuata klabu mbalimbali zilitaka saini yake lakini Mashujaa ndio iliwahi na kumsajili ambapo alikutana na ushindani wa namba.
Mwanaspoti lilifanya mahojiano na straika huyo yuko wapi kwa sasa na hapa anaeleza.
“Maisha yangu ya soka la kiushindani nilianzia Mtibwa 2019 nikacheza kwa misimu miwili baada ya hapo Mashujaa ikanisajili lakini sikufanikiwa kucheza,” anasema.
Anasema amekuwa kimya kwa takribani miezi sita akitafuta timu ya kucheza baada ya kumalizana na Mashujaa.
Anaongeza kuwa baada ya kurudi Bongo alichelewa dirisha dogo la usajili jambo lililomfanya asubiri hadi dirisha hili ndipo atafute timu.
“Kwa sasa nafanya mazoezi binafsi ya kujiandaa ikitokea kuna timu nimeelewana nayo basi nijiunge nayo lakini hadi sasa kuna ofa zaidi ya nne ninazo mkononi za ndani na nje pia,” anasema Makambo na kuongeza:
“Mpira una mambo mengi ukiachana na changamoto hiyo zipo nyingine ambazo nikisema niweke wazi basi itakuwa balaa hayo yamechangia mimi kutoonekana uwanjani.”
Anasema Oktoba mwaka jana alipata ofa kutoka Al Nasr ya Dubai kujiunga nayo lakini dili hilo likaota mbawa baada ya klabu hiyo kupigwa rungu la kutosajili.
“Ilibaki kidogo tu nisaini mkataba kila kitu ilikuwa tayari hadi nilipewa VISA ya miaka miwili lakini kumbe kulikuwa na mchezaji wa Kibrazili alipeleka kesi FIFA ya madai ya pesa aliyokuwa anawadai halafu ndio dirisha la usajili lilikuwa linafungwa siku chache,” anasema na kuongeza:
“Waliniambia nisubiri hadi dirisha lijalo nikaona haiwezekani bora nirudi Tanzania nikasikilizie ndio nimerudi napambana kuona namna gani narudi tena uwanjani na kiukweli nililia sana na nilitoka mchezoni.”
Kama angefanikiwa kucheza Dubai anaamini ndoto alizokuwa amejiwekea nje ya soka zingeanza kutimia ikiwemo kufungua maduka ya biashara mbalimbali na kuajiri vijana wenzie.
“Mshahara wangu ulikuwa Dola 10,000 sawa na Sh26 milioni kwa mwezi, niliamini nikifanikisha hilo ningewekeza mambo mengine na kusaidiana na vijana wenzangu.”
Agosti, 2023 straika huyo alikwenda nchini Denmark kwa ajili ya majaribio lakini hakufanikiwa kupita kwenye mchujo huo.
Makambo anasema alikaa mwezi mzima nchini humo na kukutana na changamoto kubwa ikiwamo wingi wa wachezaji waliokuwa wanafaya majaribio kwenye timu hiyo wakiwa 29 kutoka mataifa tofauti na waliohitajika walikuwa ni wawili.
“Kwanza kulikuwa na baridi kali sana hadi linaweka barafu ingawa baada ya siku mbili nilizoea hali ya hewa, pia vyakula ilikuwa shida lakini kulikuwa na ushindani mkubwa maana tulikuwa wachezaji 29 na wawili tu ndio walitakiwa.
“Waliniambia nisubiri ndani ya mwezi mmoja nitapewa majibu nikaona kimya, na imekuwa kama mkosi kwani sio mara ya kwanza awali nilifanya majaribio Uturuki lakini baada ya kutokea matatizo kule ya tetemeko la ardhi nikashindwa kuendelea ndio nikarudi,” anasema Makambo.
Msimu huu klabu ya Mtibwa Sugar haijafanya vizuri tangu msimu unaanza kuanzia wakubwa hadi ya vijana na hapa anaeleza wakati anapokea taarifa hizo.
“Kwanza wakati timu inafanya vibaya nilikuwa nawapigia simu wenzangu na kuwaambia pambaneni timu isishuke daraja, nikawa nawapa moyo lakini kiukweli kila kitu ni mipango ya Mungu, ikashuka,” anasema.
“Kama mdau wa Mtibwa lazima uumie, isitoshe pale ni kama akademi ya kukuza vipaji vya vijana wengi ambao wamekuwa msaada kwenye ngazi ya klabu na timu ya taifa kwa ujumla.”
Nje na biashara ndogo ndogo anazozifanya anasema hana kitu kingine ambacho anakitegemea zaidi ya soka hivyo ni kama maisha kwake.
“Msimu mzima nipo tu mtaani sina kazi lakini naishi nafanya mambo mengine, navaa nasafiri yote ni sababu ya mpira wa miguu kwahiyo ni kama soka limebeba roho yangu.”