Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa nchini kuhakikisha wanakutana na kufanya tathmini na kuweka mpango kazi wa utekelezaji Bajeti ya Wizara ya Ardhi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mhe.Pinda ametoa kauli hiyo tarehe 5 Julai 2024 wakati akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Tabora akiwa njiani kuelekea mkoani Kigoma kikazi.
Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora imeanzisha utaratibu wa kukutana na watumishi wa sekta ya ardhi wa mkoa huo kila baada ya bajeti ya wizara kupitishwa kwa kufanya tathmini na kuweka mpango kazi wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka mpya wa fedha.
Naibu Waziri wa Ardhi amesema, utaratibu unaofanywa na ofisi ya Kamishna wa Ardhi kwa kuwakutanisha watumishi wa sekta hiyo katika mkoa mzima ni mzuri na unapaswa kuigwa na ofisi nyingine za mikoa kwa kuwa unasaidia kujua muelekeo wa wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
“Huu mfumo mliouanzisha wa kukutana, kufanya tathmini na kupanga mikakati ya utekelezaji bajeti kwa mwaka mpya wa fedha ni mzuri na unapaswa kuigwa na ofisi nyingine za makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa, hiki ni kitu kikubwa katika mpango kazi wenu” alisema Mhe. Pinda.
Amempongeza kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Husein Sadick kwa kazi nzuri na ubunifu wa kukutanisha watumishi wa sekta ya ardhi ambapo ameuelezea utaratibu huo kuwa, pamoja na kujipanga kwa utekelezaji wa bajeti lakini unawezesha kujua namna ya kukabiliana na changamoto za sekta ya ardhi kwenye mkoa kwa mwaka husika.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Husein Sadick amesema ofisi yake imewakutanisha watumishi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo mbali na mambo mengine kufanya tathmini na kuweka mipango ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, vipaumbele vya Wizara ya Ardhi ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi mijini na vijijini, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji huduma na upatikanaji taarifa za ardhi, kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha mipaka ya kimataifa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda yuko njiani kuelekea mkoa wa Kigoma ambapo akiwa mkoani humo mbali na kufanya shughuli za sekta ya ardhi atashiriki ziara ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango