Hersi aongoza dua maalum ya Manji

RAIS wa Yanga, Injinia Hersi Said ameongoza dua maalumu ya kumuombea aliyekuwa mwenyekiti na mfadhili wa klabu hiyo, Yusuf Manji.

Dua hiyo imefanyika leo, makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani na kuhudhuriwa pia na ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine na viongozi wengine wa klabu hiyo.

Walikuwapo pia wazee wa Yanga wakiongozwa na mwenyekiti wao, Mohamed Msumi ambao ndio waliosimamia dua hiyo huku mashabiki na wanachama nao wakiwamo.

Manji alifariki dunia usiku wa saa sita Juni 29 jijini Florida, nchini Marekani baada ya kuugua kwa muda mfupi na kuzikwa kesho yake hapohapo.

Yanga iliandaa dua hiyo ikiwa ni kumkumbuka Manji ambaye alifanya makubwa ndani ya Yanga akiwa kama mfadhili na baadaye kuiongoza kwa nafasi ya mwenyekiti.

Wakati wa dua hiyo, mashabiki wengi walionekana kuwa na huzuni ambapo hata baada ya dua hiyo wengi walionekana kuumizwa na kifo cha bilionea huyo.

Akizungumza mara baada ya dua hiyo, Hersi amesema uongozi wao umelazimika kuandaa dua hiyo katika kuthamini mchango wa Manji ndani ya klabu hiyo.

“Dua hii ni kuthibitisha kuwa tunaenzi yale yote mazuri aliyoyafanya marehemu Manji wakati wa uhai wake, aliyoyafanya yataendelea kubaki kwenye kumbukumbu nzuri za klabu hii na hata kwenye mioyo yetu wapenda soka,” amesema Hersi.

Manji katika misimu mitano aliyokaa madarakani kuanzia mwaka 2012-2017, aliipa Yanga mataji manne ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara yakiwamo matatu mfululizo.

Related Posts