Dar es Salaam. Sakata la matibabu ya Edgar Mwakabela, maarufu Sativa aliyejeruhiwa baada ya kutekwa kwa siku nne na kutelekezwa katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi, limechukua sura ya kisiasa baada ya pande tofauti za wanasiasa kutia mguu kwenye suala hilo.
Sativa alitoweka Juni 23, 2024 na kupatikana Juni 27, 2024 akiwa amejeruhiwa hasa kwenye taya. Kijana huyo alisafirishwa kutoka Katavi kuja Dar es Salaam ambapo alifikishwa katika hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu.
Kampeni za kuchangia matibabu ya Sativa zinaendelea mtandaoni ambapo wanasiasa mbalimbali wamejitokeza kuchangia matibabu yake. Hata hivyo, bado mjadala umetawala kwenye mtandaoni wa X huku wakidaiwa kutaka kubeba ajenda hiyo.
Kwa mujibu wa mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, Rais Samia Suluhu Hassan amelipa Sh35 milioni kwa ajili ya matibabu wa Sativa ambazo inaelezwa zimeingizwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Hospitali ya Aga Khan.
Hata hivyo, suala la uchangiaji limeibua sintofahamu na mvutano ambapo baadhi ya wadau wanavutana kuhusu michango hiyo huku mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akibeba lawama kwamba anajinufaisha kisiasa katika jambo hilo.
Kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) rafiki wa Sativa, Taivina James, ambaye ndiye alibaini kutoweka kwake, Julai 4, 2024 aliandika akieleza namna suala la matibabu ya Sativa linavyotumika kuwanufaisha baadhi ya watu.
“Gharama za escort ya polisi, Ambulance na shirika la kina Wakili Kisabo ni vitu ambavyo tumekuwa tukiujulisha umma kuwa tumelipa escort (hata kwenye tweet jana niliongea), tumelipa Ambulance na gharama nyingine zikiwemo za shirika”.
James amehoji sababu za ACT Wazalendo kutoujulisha umma kuwa kuna michango wametoa wao, lakini baada ya kutangaza wametoa wao, anahoji sababu ya Zitto na wenzake wa ACT Wazalendo kujitokeza sasa baada ya wao kutangaza.
“Pili, kama picha za Zitto akiwa Aga Khan zilitoka mapema, taarifa ya Zitto kuwasiliana na Rais imetoka mapema, why (kwa nini) taarifa ya Zitto ku-deposit (kuweka) Sh10 milioni imechelewa kutoka na sisi tulikuwa tunatoa taarifa kuwa tunalipia costs (gharama) fulani na fulani?”
“Kwa sababu hata michango ya Rais ikitoka, kunakuwa na public statement official (taarifa rasmi kwa umma) kuwa Rais kachangia kiasi fulani, why (kwa nini) hii ya sasa tumeipata kupitia kwa Zitto?” amehoji kijana huyo.
Alipotafutwa kuzungumzia madai kwamba anatumia jambo hilo kujinufaisha kisiasa, Zitto amesema alifanya kila kitu kwa ajili ya kumsaidia Sativa, hivyo jambo hilo hataki liwe mjadala kwa sasa.
“Nimefanya kila kitu kwa ajili ya kuokoa maisha ya Sativa. Sina la ziada la kusema kwenye hili. Inaniumiza sana kuwa jambo hili limekuwa mjadala. Tunamuumiza tu Sativa. Naomba sana jambo hili lisiwe mjadala. Aliyesaidia kasaidia, liishe,” amesema Zitto.
Kuhusu utata uliopo kuhusu aliyechangia gharama za usafiri kutoka Katavi hadi Dar es Salaam, kati ya Zitto na familia ya wana-X, Zitto amesema katika hilo halina utata. “Hakuna utata, tazama facts utaona ukweli.”
Akizungumza na Mwananchi kuhusu mvutano huo, kaka wa Sativa, Patrick Israel hakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo, akidai kwamba atafanya hivyo muda ukifika.
“Hilo suala liko ‘pending’ kidogo, tutalizungumzia k,” amesema Patrick.
Kwa upande wake, mratibu wa michango ya matibabu ya Sativa, Martin Masese amesema kila mtu na namna yake ya kuchangia matibabu ya Sativa na Zitto kama Watanzania wengine ama wana-X wengine, naye amechangia matibabu ya Sativa kwa namna yake na pesa zake amewasilisha kwenye akaunti ya matibabu ya hospitali.
“Kwanza, huwezi kuzuia jambo la Sativa kuonekana kisiasa, tayari lipo kwenye macho ya umma na kila mtu anaweza kulitumia namna ambavyo yeye anaona linafaa, kama kuna mwanasiasa yeyote ambaye anaona kwamba jambo hilo kwa manufaa yake ni sawa kwa upande wake,”
“Hatudhani kama ni sahihi mtu yeyote kulitumia kujinufaisha kwa namna yoyote, aidha kisiasa au kifedha au kijamii kwa sababu kijana mwenzetu aliumizwa sana na wale watekaji na amefanyiwa upasuaji mkubwa na yupo kitandani mpaka sasa hivi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mratibu wa Mtandao wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa ameitaka Serikali kuanzisha chombo maalumu kwa ajili ya kuchunguza matukio ya utekaji na kupotea kwa wananchi hasa yale yanayovigusa vyombo vya dola.
Akizungumza jana wakati wa kuwasilisha ripoti ya hali ya watetezi wa haki za binadamu na nafasi ya kiraia nchini ya mwaka 2023 jijini Dar es Salaam, Olengurumwa amesema licha ya kuwepo kwa matukio ya watu kutekwa na kupotea, huku vyombo vya Dola vikihusishwa, hakuna aliyekamatwa wala kushtakiwa.
“Matukio haya yana sura mbili, wapo wanaopotea kwa kuhusisha visa vya kiraia na wapo wanaopotea kwa kuhusisha vyombo vya Dola.
“Pia wapo wanaopotea kabisa, na wengine wanarudi na waliorudi wapo wanaoongea na wengine hawaongei kabisa,” amesema.
Amesema awali matukio hayo yalikuwa yakihusisha kupotea kwa watoto zaidi, lakini miaka ya hivi karibuni yanahusisha watu wazima na hasa na hasa wale wanaharakati wanaotetea haki za binadamu.
“Ushauri wetu kwa Samia (Suluhu Hassan) awe Rais wa kwanza kuzuia matukio haya. Kwa utashi wake aliouonyesha, aonyeshe kujali, ikiwa pamoja na kuunda tume.
“Kuwe na chombo maalumu cha kuchunguza, kwa sababu wakati mwingine vyombo vya Dola vinahusishwa na havipaswi kujichunguza,” amesema.