Putin alimkaribisha Orban kiongozi rafiki zaidi katika Umoja wa Ulaya kwa Urusi katika Ikulu ya Kremlin, na mwanzoni mwa mazungumzo yao yaliopeperushwa kupitia televisheni, alisema anatarajia kiongozi huyo wa Hungary kuzungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya kama kiongozi wa sasa anayeshikilia urais wa kupokezana wa Baraza la Ulaya.
Putin ataka kuijadili Ukraine na Orban
Putin amesema anataka kujadili mambo ambayo yamejitokeza juu ya mzozo wa Ukraine na Orban, ambaye alifanya ziara nchini Ukraine mapema wiki hii.
Soma pia;Orban kukutana na Zelensky katika ziara yake mjini Kyiv
Huku hayo yakijiri, Ukraine leo imeshutumu ziara hiyo ya Orban mjini Moscow.
Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema kuwa uamuzi wa kufanya ziara hiyo ulifanywa na Hungary bila makubaliano au uratibu wowote na Ukraine.
Ukraine yasema ”hakuna makubaliano juu ya Ukraine bila Ukraine”
Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine imesema kwa nchi yao, kanuni ya ‘hakuna makubaliano juu ya Ukraine bila Ukraine’ haiwezi kukiukwa na kwamba wanatoa wito kwa mataifa yote kuzingatia hilo kwa dhati.
Viongozi wa Ulaya waishtumu ziara ya Orban
Viongozi wa Umoja wa Ulaya pia wamemshtumu Orban kwa kumtembelea kiongozi anayetafutwa kwa uhalifu wa kivita.
Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema kumfurahisha Putin hakutamzuia na kwamba ni umoja na ukakamavu pekee vitakavyofungua njia kuelekea amani ya kudumu nchini Ukraine.
Soma pia:Hungary yachukua urais wa Umoja wa Ulaya
Kwa upande wake, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo wa Ulaya Josep Borrell, amesema ziara ya Orban Moscow inafanyika katika mfumo wa uhusiano wa nchi mbili kati ya Hungary na Urusi.
Scholz asema sera ya nje ya EU sio jukumu la Orban
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza kuwa sera ya nje ya Umoja wa Ulaya sio jukumu la Orban na kwamba kuna sheria na ndio sababu urais wa Hungary wa Baraza la Ulaya sio sababu ya ziara hiyo bali shughuli zake kama waziri mkuu wa Hungary.
Stolternberg asema Orban aliiarifu NATO kuhusu ziara ya Urusi
Wakati wa mkutano na waandishi habari kabla ya mkutano wa kilele wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Washington Marekani wiki ijayo, katibu mkuu wa jumuiya hiyo Jens Stoltenberg, amesema Orban aliiarifu NATO kabla ya ziara hiyo nchini Urusi. Stolternberg amesema anatarajia washirika mjini Washington kujadili mkutano wa Orban na Putin na pia mazungumzo aliyofanya mjini Moscow.