RAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Kamishna mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda kwenda kutumia kuziba mianya ya ukwepaji kodi kwa sababu vichochochoro vyote anavijua. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Amesema Serikali ya Tanzania imechoka kunyanyasika kukopa kutoka kwa washirika mbalimbali wa maendeleo ilihali makusanyo yam waka mmoja kutoka kwenye soko la Kariakoo ni sawa na bajeti za wizara tatu.
Amesisitiza kuwa amemtoa aliyekuwa Kamishna wa mamlaka hiyo, Alphayo Kidata na kumteua kuwa mshauri wake wa masuala ya kikodi kwa sababu angeendelea kubaki huko ange-’data’.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Ijumaa wakati akiwaapisha viongozi wateule katika Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar.
Tarehe 2 Julai mwaka huu Rais Samia alimteua Mwenda kuchukua nafasi ya Kidata. Kabla ya uteuzi huo, Mwenda alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Baada ya kumuapisha leo, Rais Samia amemuagiza Mwenda kwenda kufanya vizuri kama alivyofanya ZRA.
“TRA chini ya Kidata imefanya vizuri, mapato yamekua sana. Mwaka huu wamekusanya Sh trilioni 27, mwaka janawalikusanya trilioni 24. Sitegemei kama utashuka.
“Nimemuona kwa sababu nimeona mwisho atadata, kazi kafanya nzuri lakini sio jinsi anavyoandamwa. Wewe uhuni wote uliopo TRA unaujua na inawezekana umefanywa na wewe humohumo. Mipango yote unaijua. Nenda kaizibe. Tunachohitaji ni mapato.
“Tunajichetua kukopa huku tunanyanyasika. Tuende tukanyanyue za kwetu kwa sababu tumeweka mazingira bora ya biashara. Kama mapato yatakusanywa vizuri Kariakoo kwa mwaka yataendesha wizara tatu. Lakini sasa inawezekana mnakusanya mnapeleka mfukoni,” amesema na kuongeza.
“Unaijua vizuri TRA, ulikuwa unamjua mnaibia vipi na wenzio, yale mliyokuwa mkiiba vichochoro vile kazibe, nimekuamini najua utaenda kufanya kazi,” amesema.
Aidha, amemtaka Mwenda kuwa na uso wa ukali kwa sababu baada ya kumuondoa Kidata TRA watu wanacheza ngoma toka juzi nakula pilau.
“Kama unataka kusurvive pale kageuzi uso, ukienda ukishirikiana nao nitapata taarifa zote. Kidata hakuwa mpenzi hata kwa sisi.
“Mzigo wangu unakuja Kidata pitisha… anasema mzigo haupiti hadi ulipiwe kodi, hata sisi tulikuwa hatumpendi, kwa hiyo jitayarishe na hilo. Ili kuwa mzuri kwangu niliyekuteua kanikusanyie fedha, ukitaka kumridhisha kila mtu huwezi kafanya kazi yako,” amesema.
Aidha, amemuagiza Mwenda kuhakikisha mifumo ya bandari na TRA inasomana kwa sababu Kidata atakuwa na kazi ya kumfuata mgongoni kujua anachokifanya.
Amemtaka kuhakikisha matumizi ya kutoa risiti EFD nchi nzima zinatumika.
Pia amemyaka kutumia njia sahihi na rafiki kudai kodi badala ya kufungia akaunti za wafanyabiashara.