Nairobi. Rais wa Kenya, William Ruto ametangaza kupunguza bajeti kwa Sh177 bilioni kuziba pengo litakalotokea baada ya kutosaini Muswada wa Fedha 2024.
Kupitia hotuba yake aliyoitoa Ikulu leo Ijumaa, Julai 5, 2024 jijini Nairobi amesema Serikali itawasilisha pendekezo bungeni kupunguzwa kwa matumizi makubwa baada ya kutosaini muswada uliolenga kukusanya Sh346 bilioni ikiwa ni kodi mpya.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi ya Kenya, amesema kiasi cha Sh169 bilioni za zitapatikana kupitia mkopo.
Kiasi hicho, Rais Ruto amesema kitasaidia utekelezaji wa maeneo muhimu ya bajeti ikiwamo kutoa ajira za walimu 46,000 wa shule za sekondari na msingi na ulipaji wa mafao, kuajiri wataalamu wa afya, kununua maziwa kutoka kwa wakulima Sh50 kwa lita na kutoa ruzuku ya mbolea.
“Fedha nyingine ni ya kukamilisha miradi yote ya barabara iliyosimama, malipo ya deni la kahawa, kufadhili Mfuko wa Kahawa, kampuni za sukari za umma kulipa deni kwa wakulima.
Ufadhili kwa wanafunzi wapya vyuo vikuu, malipo ya malimbikizo ya madeni kwenye kaunti, Mfuko wa Maendeleo kwenye Bunge la Kitaifa NGCDPF na mafao,” amesema.
Ikiwa ni hatua za kubana matumizi, mashirika 47 ya Serikali yatavunjwa, kusitishwa kwa sherehe za harambee kwa maofisa wote wa Serikali na kuondolewa kwa bajeti za siri katika ofisi zote ikiwamo ya Rais.
Hatua hizo zilitangazwa na Rais Ruto Ikulu jijini Nairobi baada ya maandamano yaliyoishinikiza Serikali kuondoa Muswada wa Fedha 2024 bungeni kwani unakwenda kuongeza gharama za maisha.
Kuhusu harambee, Rais Ruto amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Justin Muturi amepewa jukumu la kuandaa sheria ya kupiga marufuku maofisa wa Serikali kushiriki shughuli hiyo.
Wakati huohuo, Rais Ruto ametangaza kusitisha bajeti katika ofisi ya mke wa rais, mke wa makamu wa rais na waziri mkuu.
Pia Rais Ruto amesitisha kujazwa kwa nafasi 50 za makatibu wakuu wasaidizi ambao uteuzi wao awali ulisitishwa na mahakama.
Bunge lilipitisha sheria ya uteuzi wa viongozi hao lakini sasa kwa tamko la Rais Ruto nafasi hizo zitakoma.
Vilevile Rais Ruto amesitisha ununuzi wa magari kwenye ofisi za uwakala wa Serikali pamoja na idara zao kwa mwaka mmoja isipokuwa idara za ulinzi.
Kuhusu safari, Rais Ruto amesitisha safari zote zisizo za lazima kwa maofisa wa Serikali na kupunguza bajeti ya ukarabati wa majengo ya Serikali kwa asilimia 50.
Pia ametangaza kupunguza washauri wa Serikali ambao hivi karibuni walitumia Sh1.1 bilioni kwa kuishauri Serikali.
Amesisitiza pia watumishi wote wa umma watastaafu punde wanapofikisha miaka 60.
Alipozungumzia deni la Serikali, Rais Ruto ametangaza kuunda kikosi kazi huru kuchunguza deni hilo.
Kikosi kazi hicho kitafanya kazi kwa miezi mitatu na kuja na majibu ya asili ya deni hilo la Serikali na kupendekeza njia ya kudhibiti deni hilo kuendelea kupaa.
Habari kwa msaada wa tovuti ya Daily Nation ya nchini Kenya.