Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema Jeshi hilo leo Julai 5, 2024 limepokea taarifa za uchunguzi wa vielelezo kuhusu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda anayedaiwa kumlawiti Tumsime Ngemela.
Amesema taarifa hizo wamezipokea kutoka maabara za uchunguzi wa kisayansi.
Kamanda Mutafugwa amesema hayo saa chache baada ya Tumsime akiwa ofisi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), jijini Dar es Salaam, kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo akiomba msaada wa Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili haki itendeke.
Kamanda Mutafungwa amesema, “Kama ilivyo katika uchunguzi wa makosa ya jinai likiwamo na hili, jalada lazima lifike Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali.”
“Jalada hili lilishafikishwa katika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali na taarifa hiyo ya uchunguzi wa vielelezo hivyo kutoka maabara ya uchunguzi wa kisayansi ambazo nimesema tumezipata leo na zenyewe zinafungashwa kumpelekea Mkuu wa Mashtaka wa Mkoa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria,” amesema.
Kamanda Mutafungwa aliyekiri kuona mahojiano ya binti huyo akieleza tukio zima lilivyotokea amemtoa hofu akimuahidi uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa ukaribu, makini na weledi mkubwa.
“Nipende kumtoa hofu binti huyo na kumhakikishia uchunguzi makini na wenye weledi unaendelea, na kupitia hayo atapata haki yake ambayo atastahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, uchunguzi wa matukio hayo hauhusishi polisi peke yake. “Tunachunguza wengi… lakini katika hatua hizi tutarajie kuanzia Jumatatu Ofisi ya Mashtaka ya Mkoa itatoa mwongozo wa hatua zinazochukuliwa,” amesema
Amesema kwa sasa Dk Nawanda yupo nje kwa dhamana.
Ameeleza dhamana ni haki ya mtuhumiwa wa kosa kama lake kwa mujibu wa sheria na kwamba, Dk Nawanda anaripoti ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza.