Tamasha la Utamaduni na Utalii Kanda ya Ziwa-Lake Zone Cultural and Tourism Festival limeanza Mjini Bariadi kwa kishindo huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikisema itaendelea kuwekeza katika utalii wa utamaduni ili kuutangaza zaidi utamaduni wa Kitanzania.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula wakati wa ufunguzi rasmi wa Tamasha la Utamaduni na Utalii Kanda ya Ziwa (Lake Zone Cultural and Tourism Festival) lililoandali na kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours na litafanyika kwa siku tatu Julai 5, 6 na 7 katika Viwanja vya CCM Bariadi.
Naibu Waziri huyo aliyeongozana na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga na viongozi wengine amesema, “Wizara ya Maliasili na Utalii na Serikali kwa ujumla inaunga mkono tamasha hili la aina yake ambalo limeunganisha mambo mawili yaani utamaduni na utalii.”
Amesema watu wa Simiyu wana utamaduni wa kipekee ambao hata hivyo bado haujatangazwa vizuri ili watalii waje wajionee. “kwetu utalii ni pamoja na watanzania wenyewe kutoka pembe zote za nchi hii sio kutoka nje ya nchi tu.
Amesema kwa kushirkiana na Wizara ya Utamaduni Sanaa, na Michezo watahakikisha matangazo yatafanyika kwa namna ya kipekee.
Amesema Mkoa wa Simiyu una vivutio vingi mno vya utalii na kutoa wito kwa washiriki wa tamasha watafute muda wa kutembelea baadhi kama sio vivutio vyote.
Naye Christina Jengo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro one Travel and Tours, amesema Tamasha hilo linatarajiwa kuwaleta pamoja washiriki zaidi ya 7000 kwa siku hizo tatu.
“Tunatarajia kuwa na ngoma mbalimbali zikiwemo za makundi ya Wagalu na Wagika, kucheza na nyoka na fisi, maonesho ya biashara pamoja na vifaa vya asili na tiba,” alisema.
Pia ameshukuru wadhamini wa tamasha hilo ambao ni pamoja na NMB Bank, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), People’s Bank of Zanzibar (PBZ), Zanzibar Insurance Corporation (ZIC), Z&M General Traders, Widescope Enterprises Limited, na Carehealth and Hospitality Services. “Naamini baada ya tamasha hili la kwanza mwaka huu, mashirika mengine yataona umuhimu wa kuunga mkono tukio la mwakani maana nimearifiwa hili litakuwa tamasha la kila mwaka.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Afisa Utamaduni, Nyambeho Magesa aliipongeza kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours kwa kuunga mkono mwito wa Rais Mh. Dk Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha tamasha katika kila mkoa kwani wao wamefanya kwa vitendo.
Amesema Wizara hiyo itaendelea kufanya kazi pamoja na Kilimanjaro One Travel and Tours na Wizara ya Maliasili na Utalii kukuza utalii wa utamaduni.
Makundi mbalimbali yalipata nafasi ya kutoa burudani katika siku ya kwanza na kuwavuta mamia ya wakazi wa Bariadi huku kilele kikitarajiwa kuwa Julai 7 ambayo ni Sikukuu ya Saba Saba.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (wa tatu kushoto), na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga (katikati), wakipiga ngoma kuzindua rasmi Tamasha la Kimataifa la Utamaduni na Utalii lililofanyika katika Uwanja wa CCM Bariadi mkoani Simiyu, katika kuenzi utamaduni wa Wasukuma Kanda ya Ziwa (Lake Zone Cultural and Tourism Festival, lililoandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro one Travel And Tours. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Christina Jengo, Afisa Utamaduni wa Mkoa, Charles Maganga, Afisa Utamaduni wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Nyambeho Magesa, Mkurugenzi Mkuu wa Kilimanjaro One Travel and Tours, Mohamed Hatibu na Meneja wa NMB Bariadi, Julieth Kishamba.
Kikundi cha ngoma ya Asili ya Mwaginya kikitumbuiza katika Tamasha la Kimataifa la Umaduni na Utalii lililofanyika katika Uwanja wa CCM Bariadi mkoani Simiyu, katika kuenzi utamaduni wa Wasukuma Kanda ya ziwa (Lake Zone Cultural and Tourism Festival, lililoandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro one Travel And Tours